HabariMichezo

Buriani Kadenge

July 7th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

JAGINA wa kabumbu nchini Kenya Joe Kadenge ambaye ni mwanasoka maarufu zaidi katika historia ya mchezo huo aliaga dunia hapo Jumapili katika hospitali ya Meridian jijini Nairobi.

Kifo chake kilithibitishwa na mwanawe, Oscar Kadenge ambaye alisema mkongwe huyo aliyekuwa akiugua kwa muda mrefu alifariki akiwa na umri wa miaka 84.

“Mzee amekuwa akiugua kwa muda mrefu huku akipokea matibabu mara kwa mara. Hali yake ilididimia mara tu dadangu alipoaga dunia mapema mwaka huu nchini Amerika, na hata hakuweza kuhudhuria mazishi yake,” alisema Oscar ambaye pia alikuwa mchezaji matata wa AFC Leopards.

Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa upinzani, Raila Odinga na Musalia Mudavadi ni miongoni mwa watu mashuhuri waliowahi kumtembelea miaka ya karibuni akiwa mgonjwa.

Miaka miwili iliyopita, Rais Kenyatta alimtembelea mshambuliaji huyo mstaafu nyumbani kwake katika mtaa wa Mariakani na kumpa Sh2 milioni.

Kabla ya kujiunga na AFC Leopards (wakati huo Abaluhya United), Kadenge aliichezea Maragoli United ambayo hatimaye ilibadilisha jina na kujiita Imara United.

Kadenge anakumbukwa kama kiungo mshambuliaji matata aliyekuwa katika kikosi cha kwanza cha Harambee Stars kabla ya Kenya kupata uhuru na alikuwa kikosini hadi 1969 alipostaafu na kuanza kujishughulisha na kazi ya ukufunzi.

Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF), Nick Mwendwa ni miongoni mwa waliotuma risala zao jana baada ya kutangazwa kifo cha mkongwe huyo.

“Nimehuzunishwa na kifo cha jagina Joe Kadenge. Msaada wake na kujitolea kwake kuimarisha soka nchini utakumbukwa daima nchini na mataifa ya kigeni,” alisema Mwendwa.

“Kwa niaba ya FKF, napenda kutuma risala zangu za rambirambi kwa jamaa na marafiki huku nikiwatakia nguvu wakati huu wa majonzi.

Kadenge alikuwa katika kikosi cha AFC Leopards kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mnamo 1966 na 1967.

Mnamo 2010 alipewa fursa ya kuwakilisha Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) katika fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.

Marehemu alitunukiwa tuzo ya Balozi wa Soka Nchini Kenya mnamo 2012 kuongeza kwa tuzo nyingine ya awali ya ‘Hall of Fame’.