Habari MsetoSiasa

BURIANI MOI: Alikuwa gwiji wa kunoa viongozi chipukizi kisiasa

February 4th, 2020 3 min read

Na WANDERI KAMAU

MZEE Daniel Moi aliwajenga kisiasa viongozi wanaoshikilia nyadhifa kuu serikalini kwa sasa, miongoni mwao wakiwemo Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.

Wengine aliochangia safari zao za kisiasa ni Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kinara wa ANC Musalia Mudavadi na aliyekuwa Makamu wa Rais marehemu George Saitoti kati ya wengine.

Mzee Moi anatambuliwa kama mlezi wa kisiasa wa Rais Kenyatta tangu akiwa limbukeni, kwani ndiye aliyemtoa kwenye giza la siasa na kumjenga hadi akachaguliwa kuongoza nchi mnamo 2013.

Mzee Moi ndiye aliyemtambulisha Rais Kenyatta kwa Wakenya baada ya kumteua kama mwenyekiti wa Bodi ya Kusimamia Utalii (KTB) mnamo 1999.

Kabla ya uteuzi huo, Bw Kenyatta aliwania ubunge katika eneo la Gatundu Kusini, lakini akashindwa na Bw Moses Mwihia mnamo 1997.

Mnamo 2001, aliteuliwa kuwa mbunge maalum na baadaye Waziri wa Serikali za Wilaya. Kufuatia hilo, alichaguliwa kuwa mmoja wa wenyekiti wanne wa Kanu mwaka uo huo.

Mnamo 2002, Mzee Moi alitumia ushawishi wake kushinikiza kuteuliwa kwa Bw Kenyatta kama mwaniaji urais kwa tiketi ya Kanu. Hatua hiyo ilionekana kama njia ya kumtayarisha kuwa mrithi wake kisiasa.

Ingawa alishindwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki, aliyewania kwa tiketi ya muungano wa Narc, Bw Kenyatta alichukua usukani wa kuwa Kiongozi Rasmi wa Upinzani nchini.

Naye Dkt Ruto alisaidiwa na Bw Moi kujtosa kwenye ulingo wa siasa kupitia vuguvugu la YK ‘92 (Youth for Kanu 92) alikohudumu kama Katibu Mshirikishi.? Kundi hilo liliwashirikisha kundi la wanasiasa kutoka Kanu, ambao walikusanywa ili kumpigia debe Bw Moi kwenye uchaguzi mkuu wa 1992.

Uchaguzi huo ndio ulikuwa wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi nchini.

Kando na Dkt Ruto, Bw Jirongo pia alihusishwa pakubwa na kundi hilo, kwani ndiye aliyekuwa mwenyekiti wake.

Mzee Moi ndiye aliyeanza vuguvugu hilo, ili kurejesha umaarufu wa Kanu, ambao ulikuwa umeshuka sana nchini.

Lengo kuu la vuguvugu lilikuwa kuwashinikiza vijana kujiunga na Kanu.

Bw Jirongo alipata umaarufu mkubwa kwa kutoa mabunda ya pesa kwenye mikutano ya kampeni, kiasi kwamba baadhi ya mawaziri walidaiwa kwenda afisini mwake kuomba pesa.

Hata hivyo, ushawishi wa Bw Jirongo ulipungua baada ya uchaguzi huo, hasa baada yake kujaribu kujijenga kisiasa kwa kutumia fedha alizokuwa amepata kutoka kwa kampeni za kundi hilo.

Dkt Ruto pia alianza kulalamika kwamba Mzee Moi hakuwashirikisha vijana kwenye serikali yake licha ya kumfanyia kampeni pakubwa.

Wale waliolengwa na Dkt Ruto ni Prof Saitoti na Bw Nicholas Biwott, aliyekuwa waziri mwenye ushawishi mkubwa kwenye serikali ya Mzee Moi.

Kutokana na malalamishi hayo, Mzee Moi alivunja kundi hilo kwa kumfurusha Bw Jirongo kutoka kwa kundi la washirika wake wakuu kisiasa.

Marafiki wake wa karibu ambao walishirikiana nao kama Mabw Sam Nyamweya, Gerald Bomet na Jimmy Choge pia walijitenga naye.

Ikizingatiwa hakuwa mwenye ushawishi mkubwa ikilinganishwa na Bw Jirongo, Mzee Moi alimnusuru Dkt Ruto. Hata hivyo, Dkt Ruto alikuwa amefaulu kubuni marafiki miongoni mwa jamii ya Wakalenjin.

Dkt Ruto alitumia urafiki wake na washirika wa karibu wa Bw Moi kama aliyekuwa katibu wake Bw Joshua Kullei na mwanasiasa Mark Too kujijenga kisiasa.

Ingawa hakufahamika sana, Dkt Ruto alianza kampeni kali katika eneobunge la Eldoret Kaskazini dhidi ya mwanasiasa mkongwe Ruben Chesire, aliyekuwa mshirika wa karibu wa Mzee Moi.

Licha ya juhudi zake, wanasiasa wengi wenye ushawishi walimdharau.

Wawili hao (Jirongo na Ruto) waliendeleza harakati zao za kisiasa, hali iliyowawezesha kuchaguliwa kama wabunge katika maeneo ya Lugari na Eldoret Kaskazini mtawalia mnamo 1997.

Kwenye uchaguzi wa 2002, Dkt Ruto alichaguliwa tena kama mbunge wa Eldoret Kaskazini, huku Bw Jirongo akipoteza nafasi yake kama mbunge wa Lugari.

Dkt Ruto sasa anahudumu kwa kipindi cha pili kama Naibu Rais baada ya Chama cha Jubilee (JP) kuibuka mshindi kwenye chaguzi za 2013 na 2017. Anapania kuwania urais mnamo 2022.

Juhudi za Bw Jirongo kuwania urais mnamo 2017 kwa tiketi ya chama cha KADDU ziligonga mwamba.

Mzee Moi pia alichangia pakubwa safari ya kisiasa ya Bw Mudavadi, kwani ndiye alimteua kama Waziri wa Fedha mnamo 1993 akiwa na umri wa miaka 29 pekee.

Hili lilichangiwa pakubwa na urafiki wa Mzee Moi na babake Bw Mudavadi, Bw Mudamba Mudavadi. Bw Mudavadi pia alihudumu kama Makamu wa Rais chini ya Mzee Moi kati ya Novemba 2002 na Januari 2003.

Bw Musyoka alihudumu katika nyadhifa mbalimbali za uwaziri chini ya serikali ya Mzee Moi, huku Prof Saitoti akihudumu kama Makamu wa Rais kati ya 1989 na 1998; na 1999 na 2002.