Habari MsetoSiasa

BURIANI MOI: Alivyodumisha amani nchini huku akiwatesa wananchi

February 4th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Katika utawala wake wa miaka 24, Daniel Moi alitumia filosofia yake ya Nyayo iliyokuwa na kauli mbiu ya Upendo, Umoja na Amani kuunganisha Wakenya huku akiendeleza utawala wa kiimla.

Kinaya ni kwamba alama yake kuu ilikuwa ni rungu lake ambalo hakuacha kokote alikozuru nchini au nchi za ng’ambo.

Ingawa alisema angefuata nyayo za mtangulizi wake Hayati mzee Jomo Kenyatta, wengi walisema filosofia hii iligubikwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ufisadi na utawala mbaya, japo maeneo mengi nchini yalishuhudia amani hadi miaka ya tisini siasa za kupigania mfumo wa siasa wa vyama vingi ulipoanza kushika kasi nchini.

Wadadisi wengi wanasema kwamba Moi alitumia filosofia hiyo ili kutia nguvu utawala wake wa kidikteta huku kila Mkenya akitakiwa kufuata maagizo yake kama kiongozi wa nchi na maamuzi ya chama cha Kanu bila kumkosoa.

“Katika utawala wake wa kidikteta, raia walitakiwa kufuata maagizo yake bila kumkosoa na waliomkosoa walitupwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka. Hii ilikuwa kinyume na alivyohubiri katika filosofia yake ya Upendo, Umoja na Amani,” mwandishi Noam Chomsky kutoka Amerika asema katika kitabu chake Problems of knowledge and freedom.

Anasema kwamba waliokosoa filosofia ya Moi walilazimika kutoroka Kenya au kutoweka kabisa. Filosofia hii ilipata umaarufu mwingi hasa kwa kuvumishwa na wakereketwa wa chama cha Kanu na wanahistoria wanasema itachukua miaka mingi kuifuta.

“Moi alihakikisha kuwa filosofia yake ya Nyayo ilikita mizizi kwa kuanzisha shule na majengo yaliyopatiwa jina Nyayo, katika kila eneo Kenya kuna angalau jengo liwe la shule au wodi ya hospitali linalofahamika kama Nyayo. Hakuna asiyefahamu uwanja wa michezo wa Nyayo jijini Nairobi na jumba la Nyayo ambalo ofisi kadhaa za serikali zinapatikana,” asema Paul Muchoki 78 ambaye alikuwa afisa wa chama cha Kanu jijini Nairobi miaka ya tisini.

Sawa na mtangulizi wake, Moi alihakikisha jina lake limevumishwa kote nchini. Kuna viwanja viwili vya ndege vilivyo na jina lake katika miji ya Mombasa na Eldoret na uwanja mkubwa wa michezo nchini ulio Kasarani pia umepatiwa jina lake.

Aidha takriban katika miji yote nchini, kuna barabara iliyo na jina lake. Mjini Eldoret, kuna chuo kikuu kilicho na jina lake.

“Sio rahisi kumfuta Moi kutoka maisha ya Wakenya,” alisema Bw Muchoki. Ili kuhakikisha amedumisha umaarufu wake, Moi alikuwa akihusika katika kila shughuli ya serikali yake hadi akafahamika kama Mkenya nambari wani katika kila sekta.

Alikuwa mkulima nambari wani, mwalimu nambari wani akiwa chansela wa vyuo vikuu kote nchini miongoni mwa kusimamia shughuli ambazo zingeongozwa na mawaziri wake. Wakati mmoja alidai kuwa hata akipiga chafya Wakenya wote wanapata homa.