Habari MsetoSiasa

BURIANI MOI: Kutoka mchungaji mifugo, mwalimu hadi Ikulu

February 4th, 2020 4 min read

Na BENSON MATHEKA

DANIEL Toroitich arap Moi, aliyekuwa rais wa pili wa Kenya na kutawala kwa miaka 24, alizaliwa Septemba 2, 1924, katika kijiji cha Kurieng’wo, Sacho, wilayani Baringo akiwa mwana wa tano wa mke wa kwanza wa baba yake Kimoi arap Chebii.

Kama jina lake, Toroitich linavyomaanisha “karibisha mifugo nyumbani”, Moi alianza kuchunga mifugo kama vijana wengine wa jamii yake katika kijiji cha Kurieng’wo.

Baba yake alikufa akiwa na umri wa miaka minne na kaka yake, Tuitoek, akawa mlezi wake. Ni Tuitoek aliyemshawishi Moi kwenda shuleni akiwa na umri mdogo ili aweze kutoroka umaskini uliokuwa kwao.

Mnamo 1934, Moi alianza masomo katika shule ya Africa Inland Mission, Kabartonjo, takriban kilomita 45 kutoka nyumbani kwao.

Mnamo Oktoba 20, 1936, alibatizwa na kuitwa Daniel.

Mwaka wa 1938, alihamishiwa shule ya African Inland Mission, Kapsabet na baadaye shule ya African School Kapsabet, ambapo alikuwa kiranja mkuu na nahodha wa timu ya soka. Alifanya kazi za vibarua akiwa shuleni na nje ya shule ili aweze kukimu mahitaji yake ya kimsingi.

Mnamo 1945, Moi alichaguliwa kujiunga na shule ya upili ya Alliance katika Kaunti ya Kiambu lakini serikali ya kikoloni haikumruhusu. Badala yake, alitumwa chuo cha mafunzo ya ualimu.

Alipomaliza mafunzo ya ualimu, alitumwa Kabarnet kama mwalimu mkuu. Aliendelea kusoma kibinafsi na kufuzu mtihani wa London Matriculation Examinations.

Mnamo 1949, alipandishwa cheo na kuwa mwalimu wa kiwango cha P2 baada ya kozi fupi katika chuo cha Kagumo katika Kaunti ya Nyeri.

Alihamishwa hadi Tambach Government African School kama mkufunzi wa walimu.

Moi alimuoa Helena (Lena) Bomet mwaka wa 1950 na walijaliwa watoto wanane -mabinti watatu na wavulana watano.

Mwaka huo alihudhuria mafunzo katika chuo cha Jeans School (sasa inaitwa Kenya School Of Goverment) na baadaye akatumwa kufanya kazi katika Government African School, Kabarnet, ambako alifunza hadi 1955 alipojiunga na siasa.

Kujiunga na siasa kwa Moi kulifuatia mkutano aliofanya na kundi la wapiganaji wa uhuru chini ya uongozi wa Brigedia Daniel Njuguna aliyemtembelea Juni, 1955.

Aliunga mkono vita vyao na baada ya kuwalisha na kuwaweka salama kwa wiki mbili, aliwapa chakula zaidi na Sh500.

Mnamo Oktoba 1955, Moi alichaguliwa kutoka orodha ya watu wanane kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Joseph ole Tameno, ambaye alikuwa amejiuzulu kutoka kiti kisichokuwa rasmi katika Bunge la Wawakilishi (Legco).

Moi alipoketi Legco akiwa na wanachama wengine wanne pekee Waafrika mnamo Oktoba 18, 1955, hakujua yaliyokuwa yakimsubiri katika siasa.

Hata hivyo, alikabiliana na changamoto mpya na mnamo 1956 aliwasilisha mswada kutaka walimu Waafrika waruhusiwe kuunda chama chao wenyewe.

Chama cha Kitaifa cha Muungano wa Walimu Kenya (Knut) kiliundwa na kusajiliwa 1957.

Alishirikiana na viongozi wengine kama vile Eliud Mathu, Ronald Ngala na Masinde Muliro, kutetea Jomo Kenyatta na wenzake kuachiliwa kutoka kizuizini na idadi ya Waafrika katika Legco kuongezwa. Mnamo 1959, aliongoza kundi la viongozi kumtembelea Kenyatta kizuizini Lodwar.

Mnamo 1960, Moi na wanachama wengine Waafrika katika Legco walishiriki katika mazungumzo ya kikatiba ya Lancaster House jijini London katika maandalizi ya uhuru wa Kenya kutoka kwa Uingereza. Waliporudi nchini, walinuia kuanzisha chama kimoja cha kitaifa cha kisiasa.

Lakini tofauti kati yao zilifanya waunde vyama viwili – Kanu cha James Gichuru, Jaramogi Odinga na Tom Mboya kilichobuniwa Kiambu, na Kadu cha Ronald Ngala, Moi, Masinde Muliro na Martin Shikuku (katibu- mkuu) walichounda wakiwa Ngong.

Moi na wengine katika Kadu walikataa Kanu wakidai ilikuwa kikiwakilisha maslahi ya jamii kubwa za Waluo na Wakikuyu. Kwa hivyo, waliamua kuunda muungano wa makabila mengine.

Kwenye uchaguzi wa 1961, Kanu ilishinda viti 19 na Kadu 11. Lakini Kanu ilikataa kuunda serikali hadi Kenyatta aachiliwe huru.

Nayo Kadu ikakubali na Moi akateuliwa waziri msaidizi katika Wizara ya Elimu mnamo 1961. Baadaye alihudumu katika wizara za Elimu na Serikali za Wilaya.

Katika uchaguzi wa 1963 ambao ulileta uhuru, Kadu ilikataa kuwasilisha wagombeaji kupinga Kanu, wakati huo ilikuwa chini ya uongozi wa Kenyatta baada ya kuachiliwa kutoka kizuizini mnamo 1961.

Kadu ilishindwa na kuwa katika upinzani huku Kenyatta akichaguliwa Waziri Mkuu.

Akiwa mwenyekiti wa Kadu, Moi aliona utata wa siasa na akaamua kufuata mfumo wa umoja wa kitaifa. Hii ndiyo iliyofanya Kadu kuvunjwa Novemba , 1964.

Wanachama wake walijiunga na Kanu na Kenya ikawa taifa la chama kimoja. Kenyatta alimteua Moi kuwa Waziri wa Mashauri ya Ndani, wadhifa ambao alihifadhi hata alipokuwa Makamu wa Rais.

Wadhifa wa Mshauri wa Ndani, ulikuwa muhimu kwa sababu alikuwa akisimamia magereza, polisi na Idara ya Uhamiaji.

Kulingana na Toleo la Africa Confidential la Juni, 1990, lilisema Moi alitumia Wizara ya Mashauri ya Nyumbani kufanya urafiki na watu wengi kote nchini ambao ulimfaa miaka ya baadaye kisiasa.

Jukumu lake la kutoa paspoti lilimkutanisha na wafanyabiashara kutoka bara Asia na kampuni kutoka Uingereza.

Lilikuwa jukumu la Moi pia kuteua wakuu wa polisi, magereza na huduma za uhamiaji.

Hii ilimfaidi miaka ya baadaye wakati huduma ya polisi ilipokuwa imejaaa watu ambao Moi aliteua.| Lakini kumezwa kwa Kadu hakukutuliza siasa.

Badala yake, kulizua vita katika Kanu asilia, kati ya mirengo miwili, mmoja ukimuunga Rais Kenyatta na mwingine Makamu wa Rais Odinga.

Kufikia 1966, tofauti zilikuwa zimefikia kiwango ambacho hazingetatuliwa na wakati Odinga alipovuliwa wadhifa wa makamu wa rais katika kongamano la Limuru, alijiuzulu kutoka chama hicho na kuunda KPU.

Joseph Murumbi, aliteuliwa Makamu wa Rais lakini akajiuzulu hata kabla ya kumaliza mwaka. Mnamo Januari, 1967, Moi aliteuliwa makamu wa rais wa tatu wa Kenya akiwa na umri wa miaka 43.

Wadadisi wanasema kwamba Kenyatta alimteua Moi kwa sababu hakuwa ameunga mkono mrengo wowote katika vuta nikuvute za kisiasa kati ya Wakikuyu na Wajaluo.

Hata hivyo, katika kitabu chake “Not yet Uhuru”, Oginga alisema Moi alikuwa sawa na twiga mwenye shingo ndefu anayeona mbali.

Kati ya 1970 na 1978, kulikuwa na shinikizo apokonywe wadhifa wa makamu wa rais ili asiweze kumrithi Mzee Kenyatta moja kwa moja kwa mujibu wa katiba.

Alihudumu kama makamu wa rais kwa miaka 11 na Kenyatta alipokufa Agosti 22, 1978, alisaidiwa na viongozi wa jamii ya Wakikuyu kama vile Mwai Kibaki na Charles Njonjo kuingia mamlakani.