Habari

BURIANI WALIBORA: Kenya yamwomboleza mwandishi stadi

April 16th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

BIWI la simanzi limetanda nchini Kenya kufuatia taarifa za kifo cha ghafla cha mwandishi, mwalimu na mwanahabari maarufu, Prof Ken Walibora.

Taarifa za kifo cha Walibora, 56, ambaye aliwahi kuwa mwanahahari wa kampuni ya habari  ya Nation Media Group (NMG), zilijulikana na kuthibitishwa jana asubuhi, siku tano baada ya kufariki kwake Ijumaa iliyopita.

Hadi kifo chake, Prof Walibora alikuwa mchangiaji mkuu wa makala ya Lugha, Fasihi na Elimu katika gazeti hili la Taifa Leo na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Riara, Nairobi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi katika eneo la Nairobi, Bw Philip Ndolo, Prof Walibora aligongwa na matatu kwenye barabara ya Landhies, Nairobi Ijumaa ya Aprili 10, 2020.

Msomi huyo ambaye anafahamika mno kwa kitabu chake cha ‘Siku Njema’ alitoweka wiki iliyopita, na tangu wakati huo, alikuwa akitafutwa na familia, marafiki, jamaa na baadhi ya wafanyakazi wenzake bila ya mafanikio.

Baada ya kupata ajali alipokuwa akivuka barabara ya Landhies karibu na kituo cha magari cha Machakos Country Bus, Prof Walibora alipelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Nairobi na akatambuliwa kwa baadhi ya stakabadhi alizokuwa nazo.Aliaga dunia baada ya saa chache na mwili wake kuhifadhiwa katika mochari ya hospitali hiyo.

Mbali na kufanya kazi katika kampuni ya NMG akiwa mwandishi wa Taifa Leo, mhariri wa kituo cha runinga ya NTV, mtangazaji wa iliyokuwa runinga ya QTV na hatimaye Mkuu wa Ubora wa Kiswahili hadi Januari 2017, Prof Walibora amewahi pia kushiriki mafunzo katika shirika la habari la Deutsche Welle (DW) nchini Ujerumani na kufundisha katika Vyuo Vikuu vya Madison-Wisconsin na The Ohio State University, Amerika alikojipatia shahada za uzamili na uzamifu (PhD) katika Fasihi ya Kiafrika.

Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Nation Media Group, Bw Stephen Gitagama alituma risala za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa Prof Walibora na akawataka madereva wawe waangalifu barabarani.

“Tumempoteza bingwa wa lugha kupitia ajali. Dereva aliyemgonga angalikuwa mwangalifu, tusingalipatwa na pigo hili. Kwa niaba ya familia pana ya NMG, natoa rambirambi zangu kwa familia na Mola amweke pema penye wema,” akasema.

Alimsifu Prof Walibora kwa uelekezi wake katika NMG uliofanikisha kuanzishwa kwa mtandao wa Swahilihub na Kiswahili kikaimarika sana katika kampuni hiyo aliyojiunga nayo upya alipotoka Amerika.

“Alikuwa mtangazaji shupavu aliyekirimiwa kipaji na umilisi mkubwa wa Kiswahili. Hakupenda kuona yeyote akichafua lugha. Alikuwa askari mlinzi wa usanifu wa Kiswahili,” akasema Bw Gitagama katika kauli iliyoungwa mkono na mhariri wa Taifa Leo, Stephen Musamali ambaye kwa upande wake, ameisihi serikali kufanya hima na kuunda Baraza la Kiswahili la Kenya kwa heshima ya Walibora.

Kwa upande wake, Mhariri Mkuu wa Taifa Leo, Bw Peter Ngare alisema: “Kwa niaba ya waandishi na wahariri wa Taifa Leo, tunamuomba Mungu aifariji familia ya Ken wakati huu wa msiba. Kama Taifa Leo, tumempoteza mwalimu na mwandishi shupavu.”

Naye Mhariri Msimamizi wa Kitengo cha Michezo katika NMG, Elias Makori alisema: “Namkumbuka Prof Walibora kwa kukubali mwaliko wangu na kuitembelea shule ya St Peter’s Nyakemincha, Nyamira nilikosomea. Aliwapa wanafunzi motisha, akawahamasisha walimu na kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili shuleni humo.”

Walibora alikuwa mhimili katika runinga ya QTV iliyofungwa na NMG mnamo 2016. Zaidi ya kutangaza taarifa za habari kila Jumamosi na Jumapili, alikuwa pia mwendeshaji wa kipindi ‘Sema Nami’.

Alikuwa miongoni mwa waasisi wa kitengo cha Kiswahili katika runinga ya Nation TV mnamo 1999 akishirikiana na Ali Mtenzi, Swaleh Mdoe na Lolani Kalu.

Aidha, alihusika pakubwa katika uzinduzi wa mradi wa usomaji wa magazeti shuleni (NiE) unaoendeshwa na NMG.

Zaidi ya Siku Njema, ameandika vitabu vingi vya kiada na vya kibunifu, zikiwemo diwani za mashairi, tamthilia na riwaya.

Baadhi ni Mbaya Wetu, Kufa Kuzikana, Ndoto ya Almasi, Kidagaa Kimemwozea, Ndoto ya Amerika na Nasikia Sauti ya Mama.

Amechangia pia katika uhariri na uandishi wa hadithi fupi katika mikusanyiko mingi ikiwemo Damu Nyeusi, Tumbo Lisiloshiba, Maskini Milionea, na kadhalika.