Makala

BURUDANI: Amefuata asili ya upande wake wa nchi jirani kuinua kipaji chake

May 23rd, 2020 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MSANII aliyechanganya damu ya Mkenya na Mtanzania, anasema fahari yake ni kwamba amefuata asili ya upande wake wa nchi jirani kuinua kipaji cha uimbaji wake.

Rajabu Sylvester almaarufu Rajah TZ anasema upande wake wa asili ya Tanzania unampa ujasiri na hivyo kujivunia talanta ya muziki.

Ana matumaini makubwa ya kuitingisha dunia miaka michache ijayo.

Anaamini kuwa na mama Mtanzania ambako kuna wanamuziki wengi mashuhuri, naye atafuata nyayo ya wanamuziki mahiri walioko huko japo yeye ni raia wa Kenya kutokana na babake kuwa Mkenya.

Mbali na hivyo, Rajah TZ alijitosa katika fani ya muziki na anaoanisha hili na hali halisi kwamba koo za babake na mamake zote zilikuwa ni za wasanii wa nyimbo za kitamaduni.

Anaamini yeye kutia zingatio katika muziki wa Karne ya sasa, atafanikiwa na kuwa maarufu sawa na walivyo wasanii wengine mashuhuri.

“Ninafanya bidii niweze kufikia kiwango cha mwimbaji mashuhuri Afrika na duniani, Diamond Platnumz. Naamini kwa uwezo wa Mungu nitafika mbali kimuziki na kutambulika sehemu nyingi za dunia,” akasema Rajah TZ.

Mwimbaji huyo alizindua kibao chake cha kwanza cha ‘She Got A Gwan’ mwaka 2017 ambapo alimshirikisha Mr Speed.

Alikirekodi kibao hicho katika studio ya One Blood One (OBO) Production iliyoko mjini Mwatate.

Baada ya nyimbo yake hiyo ya kwanza, msanii huyo aliungana na wenzake wawili, Medy Shine na Kide Spy kuwa katika kikundi cha Maninja wakatoa ngoma ya ‘Wine up’ aliyoirekodi mjini Moshi nchini Tanzania, produsa akiwa Man Mosse.

Mwanamuziki Rajabu Sylvester ‘Rajah TZ’. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Alifanikiwa kutoa audio na video vilevile za wimbo ‘Sakata’ ambao ulipokelewa vizuri na ambao unatumiwa mara kwa mara na Channel ya Y254.

Akatoa kibao kingine cha ‘Amina’ ambacho alimshirikisha mwimbaji wa Injili Lil Shedy.

“Ni kawaida yangu kumtanguliza Mungu kwani hata kama sijafanikiwa kwa lengo langu, sina haraka; najua nitafika wakati Mungu atakaponijaalia,” akasema Rajah Tz anayeimba nyimbo zake kutumia mitindo ya Bongo Fleva, Dancehall na Hiphop staili ya Gengetone.

“Nimeamua kuimba nyimbo zangu kwa kutumia mitindo hiyo sababu ndiyo inayoitikiwa zaidi na wapenda muziki hasa wale wa kanda hii ya Afrika Mashariki na hata barani Afrika kwa jumla,” akasema.

Wasanii anaofuatilia nyimbo zao ni Otile Brown, Masauti, Nyashinski, Sauti Soul na Heart_the_Band.

Nje ya Kenya, Rajah TZ ni shabiki wa wasanii wa Tanzania kina Diamond, Ali Kiba, Konde Boy, Jux na Marioo.

“Hao ndio wasanii wanaonikosha na ambao najaribu kufanya bidii kufikia viwango vyao,” akasema.

Kwa wakati huu, msanii huyu anajitayarisha kupanga kuzindua nyimbo zake mbili ambazo ana uhakika nazo zitapendwa na mashabiki wa muziki katika nchi mbili hizi; Kenya na Tanzania.

Nyimbo hizo ni ‘Kukere’ na ‘Corona’ ambayo inaelimisha na kuhimiza watu kuchukua tahadhari na gonjwa la corona ambalo linaendelea kutikisa dunia.

Kitu ambacho Rajah TZ anatamani na anacholenga kufanikiwa nacho ni kuwa msanii wa kutajika kote duniani na kwa hilo anaamini atalifikia. “Nina matumaini makubwa iko siku nitafanikiwa kuwa msanii mwenye kutajika kote ulimwenguni,” akasema.

Akieleza mapenzi yake kwa kuimba, Rajah TZ anasema alipokuwa anaimba akiwa shule ya msingi, walimu wengine walimuona kuwa sawa na wahuni lakini aliwafanya wageuze mawazo yao na kumuona kuwa kijana anayetaka kufikia lengo lake la kuwa mwimbaji mashuhuri.

“Niliingiwa na hamu ya kuwafanya walimu wasiwe na fikra kuwa msanii ni mtu mhuni. Mimi ni msanii mwenye nidhamu na ninayetaka kufikia malengo yangu ya kuwa maarufu sawa na wale ambao wakati huu wanatambulika,” akabainiosha wakati wa mahojiano.

Rajah TZ alianza safari yake ya kutaka kuwa msanii wa kutambulika alipokuwa shule ya msingi ambapo alikuwa akiimba nyimbo zilizokuwa zimeshaimbwa na wasanii waliokuwa maarufu.