Makala

BURUDANI: Babu Tale kampongeza Sai Kenya kwa ufundi wake katika tasnia

May 12th, 2020 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

ANAJIVUNIA kwa kutambuliwa na kumvutia Babu Tale, meneja wa msanii mashuhuri Diamond Platnumz kwa kuiga wimbo wa msanii Marioo kutoka Tanzania.

Gie Grace Msafwari almaarufu Sai Kenya ameuimba wimbo wa ‘Raha’ kwa mvutio wa aina yake na ambao umewafanya wapenda muziki wengi waushabikie.

Kwa muda wa kipindi cha mwezi mmoja pekee, kibao hicho cha ‘Raha’ kimeweza kuvutia mashabiki zaidi ya 268,000 katika mtandao wa YouTube na miongoni mwa wale walioushabikia ndiye huyo Babu Tale pamoja na meneja wa mwimbaji wa Tanzania Marioo, Dady Mwambe.

“Ninajivunia kuanza kuimba wimbo huo kupitia kwa produsa wangu Shirko na nimefurahi zaidi kupongezwa na kuongea na Babu Tale kwani kumenipa moyo mkubwa wa kuendeleza kipaji cha uimbaji wangu,” akasema Sai Kenya.

Msanii Sai Kenya anasema amefurahia mno kuona wimbo wake wa pili ‘Mama’ ambao umeimbwa na Harmonize alioutoa Aprili 18, 2020, na ambao hadi Mei 10 tayari ulishabikiwa na mashabiki zaidi ya 20,200.

Mwanamuziki Gie Grace Msafwari ‘Sai Kenya’. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Sai Kenya alionyesha mapenzi yake kwa muziki wa Bongo kwani wimbo wa tatu aliouimba ni wa cover wa ‘Kwaru’ wa Zuchu ambao umesambaa kwa kasi ukiwa tayari umesikizwa na wapenzi wa muziki 60,571 kutoka Aprili 26 hadi Mei 10, 2020, kipindi cha siku 14 pekee.

“Jinsi nilivyoshabikiwa na wapenda muziki na mafunzo ninayopewa na produsa wangu Shirko, sina shaka nitapiga hatua ya kuendeleza kipaji cha uimbaji wangu,” anatamba msanii huyo chipukizi mwenye umri wa miaka 19.

Ingawa wazazi wake wawili hawako pamoja, lakini Sai Kenya anashukuru kuwa baba na mama wote wanamuunga mkono na kumpa moyo wa kuendeleza kipaji chake.

“Nimeingiwa na moyo zaidi sababu wazazi wangu wako pamoja nami katika safari yangu ya mafanikio,” akasema.

Kwa wakati huu, anapanga na Shirko kutoa wimbo wake mwenyewe na anapendelea kupata msaada yeye na timu yake kufanikisha safari yake ya kuinua zaidi talanta yake na nia ya kuwa mmoja wa waimbaji mashuhuri duniani.

Kwake Sai Kenya, ana hamu kubwa ya kupata fursa ya kufanya kolabo na waimbaji wenye majina makubwa wakiwemo kina Nandy, Zuchu, Aslay, Mbosso na Marioo (Watanzania), Nadia Mukami, Akeelah, Adasa, Elani, Amoury, Ally Mahaba na Masauti.

“Kama nitapata fursa ya kuimba na waimbaji hao, nina hakika nitapata umaarufu sawa na wao. Hamu yangu kubwa ni kuhakikisha uimbaji wangu unapanda kwa kila kibao nitakachotoa maana ndipo wapenzi wa muziki wanaponishabikia zaidi,” akasema.

Anasema alipenda kuwa mwimbaji tangu alipokuwa shule za nasari na msingi akiwa kiongozi wa kundi la kwaya la shule alizosoma.

Mwanamuziki Gie Grace Msafwari ‘Sai Kenya’. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Shirko anasema kuwa Sai Kenya ni chipukizi ambaye ana nyota kali ya kupendwa na mashabiki wa muziki kutoka nchi mbili tofauti za Kenya na Tanzania; tukio ambalo alilitaja kuwa ni la ajabu sana kutokea kwa msanii chipukizi.

“Kwa maoni yangu, nina imani kubwa msanii huyu atafika mbali akiendelea na nidhamu aliyoanza nayo pamoja na bidii ya kupenda kuimba. Nikiwa mwalimu wake wa muziki na produsa, nitaendelea kumsaidia na kumpa mwongozo kwenye safari yake ya sanaa ya muziki.

“Si peke yake bali nahakikisha hii ni kwa wasanii wote wenye vipaji ambao watakuwa mikononi mwangu, nitawasaidia kadri ya uwezo wangu,” akasema Shirko.

Anatoa wito kwa washika dau washirikiane naye kusaidia kuinua vipaji vya wasanii chipukizi waonekane na kutambulika.

“Wako wengi sana lakini hawana uwezo, na mimi peke yangu sitaweza kujikimu kuetekeleza yote,” akasema Shirko.