Makala

BURUDANI: Freyzee Lovesea, msanii ambaye kazi zake zinakitangaza kisiwa cha Lamu

December 7th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

MSANII James Kabuu Ayub almaarufu Freyzee Lovesea ameibuka kupendwa na wengi ndani na nje ya Kaunti ya Lamu.

Msanii huyu chipukizi ametambulika zaidi katika tasnia ya muziki hasa kufuatia kibao chake kwa jina ‘Mtoto wa Lamu-Msondo,’ ambacho kinaelezea kwa kina kuhusiana na tamaduni na desturi za Lamu ambazo ni tofauti na zile za maeneo mengine ya nchi.

Katika wimbo huo wa Mtoto wa Lamu-Msondo, msanii Freyzee Lovesea anaeleza kwamba Lamu ni Tamu kwa wale wanaopenda ziara za kujifurahisha nafsi zao japo anaonya kuwa lazima wanaotembelea eneo hilo kuwa makini ili wasikiuke mila na tamaduni za eneo hilo.

Msanii huyu anaeleza kuwa huku wananchi wa maeneo mengine ya Kenya wakikimbilia kujivinjari kwa Pizza, katika eneo la Lamu, hali ni tofauti kwani utajiburudisha kwa Wali wa Nazi na kisha kubugia Supu ya Pweza kama kishushio.

Pia anagusia kuhusu mavazi kwa wale wanaoishi au kuzuru Lamu, akisisitiza kuwa wanawake eneo hilo huvalia buibui na madera na kwamba kuvaa minisketi ni kuhujumu mila na desturi za Lamu kwani hairuhusiwi.

Isitoshe, ufikapo kaunti ya Lamu, utapanda vyombo tofauti vya usafiri kama vile boti, mashua na punda.

Katika wimbo wa Mtoto wa Lamu-Msondo, msanii Freyzee Lovesea pia anataja mazoea ya wazee wa Lamu ambao wana desturi ya kucheza bao la kete huku akionya kuwa kama mtalii, usidhubutu kuwatatiza wazee hao wanapojiburudisha kwa mchezo huo kwani kufanya hivyo ni mwiko.

Hakusahau kutaja msemo wa tangu jadi unaoitambulisha Lamu wa ‘Ambacha Ukucha, Punda Uyao,’ kumaanisha kuwa mara nyingi punda hupitapita kwenye vishoroba vya mji wa Lamu mbio na kwa sababu hiyo, itakulazimu wewe mwenyeji, mgeni au mtalii kuwapisha wanyama hao kwa kujishikanisha na ukuta.

Ni kutokana na wimbo huo ambao umejikita katika tamaduni, mila na desturi za Lamu ambapo msanii Freyzee Lovesea amekuwa akipokea mialiko chungu nzima ili kuburudisha umma.

Miongoni mwa hafla ambazo msanii huyo hualikwa kila mara kutumbuizwa ni pamoja na zile za kisiasa, vijana, kijamii, ikiwemo hafla ya kila mwaka ya Utamaduni wa Lamu, Maulid ya Lamu miongoni mwa sherehe zingine.

 

 

Msanii mwenye umaarufu Lamu, James Kabuu Ayub (kulia), 22, kwa jina la Msimbo Freyzee Lovesea. Anatamba kwa kazi yake Mtoto wa Lamu-Msondo inayotambulisha mila na desturi za Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Freyzee Lovesea alizaliwa Mei 22, 1998, katika hospitali ya King Fahad mjini Lamu na kwa sasa ana umri wa miaka 22.

Alianza mziki akiwa mdogo kwa kuimba kwaya kanisani kabla ya kupalilia kipaji chake cha muziki zaidi punde alipojiunga na shule ya upili ya Bakanja iliyoko eneo la Mpeketoni alikosomea kati ya 2011 na 2014.

Anasema ushawishi wa wasanii walioibuka wakiwa na umri mdogo ndio uliomsukuma na kumshawishi kuingilia masuala ya muziki.

Kwa sasa anaishi eneo la Hindi lililoko Lamu Magharibi.

“Lovesea kwa Kiswahili inamaanisha ‘Bahari ya Upendo.’ Niliafikia kuchagua jina hilo kwani huwa niko mstari wa mbele kuhamasisha umma kuhusiana na upendo wa kila mmoja wetu. Pia nilijiunga na muziki ili kuleta fikra mpya katika tasnia ya muziki Kenya na Afrika na mahsusi zaidi kuitambulisha Lamu duniani,” anasisitiza msanii huyo.

Kwa sasa anatamba na vibao vinne, ambapo mbali na Mtoto wa Lamu-Msondo kilichompa umaarufu mkubwa, vibao vingine ni pamoja na Bring It On, Love You More, na Amenitenda Mema.

 

Msanii mwenye umaarufu Lamu, James Kabuu Ayub, 22, kwa jina la Msimbo Freyzee Lovesea. Anatamba kwa kazi yake Mtoto wa Lamu-Msondo inayotambulisha mila na desturi za Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Msanii Freyzee Lovesea alizaliwa katika familia ya watoto watatu, yeye akiwa wa pili.

Katika familia hiyo, ni yeye pekee ambaye ameibuka kuwa msanii japo anasema kunao ndugu zake wengine ambao wanapenda sana muziki.

Anasema safari yake ya usanii haijakuwa mteremko kwani changamoto nyingi zimemkumba, ikiwemo ukosefu wa hela hasa za kujisimamia kutekeleza miradi mbalimbali ya mziki na kujitafutia soko.

Aidha anapania kuwa kama msanii wa Bongo Flava, Diamond Platnumz ambaye anamtaja kuwa mwenye mchango mkubwa katika kubadili tasnia ya mziki wa Afrika Mashariki.

Anatoa wosia kwa vijana, ikiwemo wasanii wenzake chipukizi kutovunjika moyo na badala yake watia juhudi zaidi maishani.