Michezo

Burudani Kakamega Homeboyz ikiumiza nyasi dhidi ya Vihiga United

February 21st, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

 WAPENZI wa soka Magharibi mwa nchi wikendi hii watakuwa na burudani ya kipekee kwenye debi kali ya KPL kati ya timu ya Kakamega Homeboyz na Vihiga United itakayosakatwa Uwanjani Bukhungu kaunti ya Kakamega.

Vijana wa Kocha Francis Baraza Homeboyz wanauzoefu mkubwa katika ligi ikilinganisha na wenzao Vihiga United waliokwea ngazi kushiriki ligi kuu mwisho wa msimu jana tu.

Awali Vihiga wanaongozwa na kocha Edward Manoa walikuwa wakitesa kwenye  ligi ya chini ya Super League.

Kulingana na naibu kocha wa Vihiga Francis Xaviour, wataichukua mechi hiyo kama nyingine tu za ligi licha ya presha waliyonayo ya kutwaa ushindi.

 “Homeboyz ni timu ngumu na tunatarajia upinzani mkali kutoka kwao lakini tutawakabili kwa lengo la kupata ushindi,” akasema kiungo huyo wazamani wa AFC leopards.

Vihiga United kwa sasa wamezoa pointi mbili kwenye ligi baada ya kupata sare mbili na kupoteza mchuano moja.Kwa upande wao Kakamega Homeboyz wamezoa pointi nne na wako kwenye nafasi ya tisa ligini.

Baadhi ya wachezaji mahiri kwenye kikosi cha Homeboyz ni mshambulizi matata Allan Wanga na James Situma ambao wanatarijiwa kuwa mwiba kwa ngome ya ulinzi ya Vihiga.

Timu hiyo inayodhaminiwa na Mfanyibiashara maarufu Bw Cleophas Shimanyula imeshuhudia ufufuo mkubwa na imekuwa kipenzi cha mashabiki wengi kutoka kaunti ya Kakamega baada ya klabu ya Western Stima kuteremshwa ngazi.