Makala

BURUDANI: Larota aweka zingatio katika kuimba nyimbo za mawaidha kwa wanaume

October 5th, 2020 2 min read

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

NI waimbaji wachache wanaokutana na visanga vya mateso kutoka kwa wapenzi wao na kutoa vibao ambavyo vitawapa mafunzo wapenzi wa wanawake wenzao ama kuwapa mawaidha wanaume wasitekeleze maovu kwenye mapenzi yao.

Kuna waimbaji wanaoimba nyimbo zenye mawaidha ya busara na yenye kuwafanya wasikilizaji wa nyimbo hizo wavutiwe nazo lakini sio kuwa mawaidha hayo yanapendeza ila wanapendelea mahadhi na ala zilizotumika katika nyimbo hizo.

Kwa Laurriette Rota almaarufu Larota ni msanii aliyeanza kwa kuimba nyimbo za kujiburudisha kwa densi lakini baada ya mateso aliyopata kutoka kwa mpenzi wake wa awali, aliamua kuimba nyimbo nyingi zaidi zenye mawaidha.

“Nilianza kuimba kwa kujiburudisha na kuwaburudisha mashabiki wangu, lakini baada ya kukabiliana na mateso kutoka kwa mpenzi wangu wa awali, niliamua kuimba nyimbo nyingi za mawaidha ya kimaisha ili watu waweze kujinasua na matatizo mimi nimepitia,” akasema Larota.

Msanii huyo alipendelea kuimba tangu alipoinukia akiwa shuleni huku marafiki zake wa shule wakimsisitiza achukulie fani hiyo ya muziki kwa uzito kwani alikuwa na sauti ya kuvutia.

Larota. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Baada ya kikwazo kikubwa kutoka kwa mama yake, Larota alifanikiwa kumsihi mzazi wake huyo na hata kumsaidia kuzindua wimbo wake wa kwanza wa ‘Morning light’ mnamo mwaka 2012 aliouimba kwa mtindo wa Trance.

Larota anasema wimbo huo wa ‘Morning light’ haukuitikiwa vizuri hapa nchini lakini ulifanya vizuri zaidi kwenye mitandao ya Sound Clouds na Reverbnation ambayo yote ni ya huko ng’ambo. Baada ya kuimba nyimbo hiyo, Larota alitoa nyimbo zikiwemo ‘Moving on’, ‘Moyo wangu’, ‘National party’ na ‘Hera’.

Lakini kwa kipindi kifupi, mpenzi wake huyo alianza kuumiza moyo wake kwa kumpa vikwazo kadhaa kikiwemo kile cha kumtaka achaguwe kuendelea kuwa mpenzi wake ama kuepukana naye abaki kuwa mwanamuziki.

“Kama mpenzi wangu huyo angeliendelea kunipa mapenzi tuliyoanza naye, ningeliacha kuimba lakini alikuwa ameanza kunionyesha vitendo vya kinyama ambavyo vilinifanya nichukue uamuzi wa haraka wa kuepukana naye,” akasema Larota.

Larota aliamua kupumzika kabla ya kurudi tena mwaka 2017 kutokana na kupata sapoti kamili kwa mume wake aliyenaye pamoja na familia yake. “Namshukuru mume wangu na familia kwa kusimama nami katika kuendeleza kipaji cha uimbaji wangu,” akasema.

Tangu arudi tena katika fani ya muziki, Larota amekuwa akiimba nyimbo za mawaidha huku kwenye nyimbo nyingine akiwasihi wapendanao wawe wakiaminiana na kufurahishana na wala si kutesana.

Baadhi ya nyimbo alizoimba ni ‘Jongolo’, ‘Mimi na wewe’, ‘Gimidwaro’ na ‘Bora’. Kwa sasa anajitauyarisha kutoa vibao kadhaa ambazo prodyusa ni Teknix wa Kubwa Studio. “Ninaamini mashabiki watazifurahikia,” akasema.

Larota anasema hapendi kuvaa nguo za kuonyesha mwili wake sababu ya kujiheshimu yeye na familia yake. “Kama mzazi nataka niwe mfano mwema kwa wasichana wanaotaka kuingia katika muziki wajiheshimu kwa kuvaa nguo za heshima,” akasema huku akiwataka waimbaji waimbe nyimbo za kusaidia jamii.

Kama kuna wasanii anaowapenda ni Sanaipei Tande na Tiwa Savage na nia yake kubwa ni kutaka kufikia viwango walivyonavo Tiwa Savage na Yemi Alade.

Larota amewahi kufanya shoo nyingi jijini Nairobi hali mjini Mombasa, amekuwa na shoo yake mwenyewe ya ‘Art against Abuse’ ambayo aliizindua mnamo mwezi wa Desemba 2019 katika ukumbi wa Little Theatre.

“Ningependa kuwaambia mashabiki wangu wajitayarishe na kusubiri kupata vibao vyangu vipya hivi karibuni kwani nina uhakika watazipokea vizuri. Nina nia kubwa ya kuwaletea nyimbo zile wazipendazo.