BURUDANI: Mwigizaji mahiri na mwalimu wa Kifaransa

BURUDANI: Mwigizaji mahiri na mwalimu wa Kifaransa

NA JOHN KIMWERE

ANAELEKEA kutinga miaka minne tangia aanze kujituma kwenye masuala ya filamu.

Anaamua kujiunga na maigizo baada ya kumtazama kazi yake Angelique Boyer ambaye hushiriki filamu za Telenovela. Kando na uigizaji, Dorine Aoko Anne ni mwalimu ambaye hufunza Kifaransa kwenye shule za msingi.

”Ingawa sijapata umaafuru sana ukweli ni kuwa ninapenda uigizaji na tayari umekolea kwenye damu,” anasema na kuongeza kuwa ndani ya miaka ijayo analenga kuwa staa mkubwa barani Afrika.

Pia anadokeza kuwa ndani ya kipindi hicho anaamini kipindi chake ‘The One’ ambacho yeye hukiandaa kwenye mtandao wa YouTube kitakuwa kimepata umaarufu.

Mwanzo wake alijiunga na kikundi ambacho hufahamika kama Heroes walipokuwa wakizalisha filamu kupitia mwongozo wa vitabu vya kutahiniwa shuleni yaani setbooks. Pia amefanya kazi na kundi la Changamka Africa.

Anadokeza kuwa ndani ya miaka mitano analenga kufikia upeo wa waigizaji mahiri duniani kama Jennifer Winget na Angel Locasin wazawa wa India na Ufilipino mtawalia.

Anajivunia kushiriki filamu nyingi tu kama: Selina, Kina, Maempress, Andakava, Single kiasi, Scars na Hullabaloo kati ya nyingine.

Baadhi yazo zimepata mpenyo na kupeperushwa kwenye runinga ikiwamo ‘Varshita’ (Maishamagic), ‘Pieces of Us’ (NTV), ‘Majuto’ (Switch TV).

Hata hivyo anakiri kuwa kwenye filamu zote hajawahi kupata nafasi kama mhusika mkuu.

Mwigizaji chipukizi,  Dorine Aoko Anne. PICHA | JOHN KIMWERE

Wakenya wengi hupenda kutazama filamu za kigeni kama Nollywood (Nigeria) na Afrika Kusini bila kusahau Bongo Movie (Tanzania). Kuhusu hilo anasema ingawa wakenya wanapiga hatua bado hawajaiva katika masuala ya uigizaji.

”Filamu zetu hazina ubora kama kazi za wenzetu kutoka mataifa hayo kwa kuzingatia huzalishwa kwa gharama ya chini,” akasema.

Anasema kuwa barani Afrika angependa kufanya kazi na wasanii kama Pearl Thusi mzawa wa Afrika Kusini aliyeshiriki filamu kama Queen Sono na Catching Feelings kati ya nyingine.

Pia mwana maigizo wa Tanzania Nelly Kamwelu aliyeigiza filamu ya ‘Huba’ na ‘Women’. Na nchini Kenya angependa kujikuta jukwaa moja na Catherine Kamau ‘Sue and Jonnie’ na pia Brenda Wairimu ‘Disconnect’ na ‘Monica’.

Anasema tangia akiwa mtoto alipania kuhitimu kuwa mpishi, prodyusa wa filamu ama mhudumu kwenye ndege.

Anashikilia kuwa katika sanaa mtoto wa kike hupitia changamoto kibao kama hajapata mashiko.

”Sio kuchoma ila ni ukweli wa mambo kwa wasanii wanaokuja baadhi ya maprodyusa wana tabia mbaya ya kuwaomba mzinga wa asali ili kuwasaidia kupata umaarufu. Lakini dada akibania tu, hunyimwa ajira,” anasikitika.

Katika mahusiano ya kimapenzi anasema yupo singo wala kamwe hawezi kuweka katika kaburi la sahau kuwa amewahi kulia baada ya kutemwa na mpenziwe.

Wasanii hudaiwa kuwa wenye wapenzi kibao ambapo upande wake anasema hiyo ni kasumba ya wanadamu wala sio ukweli lakini inapaswa kueleweka kuwa nao pia wana hisia kama wengine.

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu mahiri na mwandishi stadi

Polisi wachunguza Mbogo kwa madai ya uchochezi

T L