Makala

BURUDANI: Valary mwigizaji chipukizi kuandaa shindano la urembo wikendi mtaani Kayole

December 14th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

WAHENGA hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa, waliposema kuwa penye nia pana njia, maana ndivyo ilivyo tangia zama hizo na ipo hivyo mpaka sasa.

Usemi huo umeonyesha mashiko ya haja miongoni mwa jamii. Aidha ni msemo unaozidi kudhihirishwa na wengi ambao wameamua kujituma kisabuni kwa kujiamini wanaweza kusudi watimize malengo yao maishani.

MISS NA MR

Valary Akinyi ni miongoni mwa waigizaji wanaozidi kuvumisha tasnia ya filamu nchini ingawa bado hawajashika mashiko. Licha ya janga la corona kupiga stopu shughuli nyingi duniani, msanii huyu kupitia brandi yake ‘Nawiri Arts Productions’ ameandaa shindano la vijana kutafuta Miss na Mr Lower Savannah mtaani Kayole, Nairobi. Shindano hilo litafanyika Jumamosi ya wiki hii na linatarajiwa kuvutia wafuasi wengi katika eneo hilo.

”Tunalenga kukuza talanta za vijana mitaani huku tukidhamiria kutumia shindano hilo kuwasaidia kujihepusha dhidi ya matendo maovu,” dada huyo alisema na kuongeza kuwa ndani ya kipindi hiki wengi wamejikuta njia panda kwa kukosa ajira.

Dada huyu anasema shindano hilo litajumuisha jumla ya washiriki 20, wasichana kumi sawa na wavulana ambapo washindi tatu wa kwanza katika kila jinsia watatuzwa. Msanii huyu anashukuru wenzake wanaoibuka na wazo hilo linalenga kusaidia vijana wa eneo hilo kutambua talanta zao katika masuala ya urembo. Akinyi, 27, ameandaa shughuli hizo akishirikiana na wenzako akiwamo Rael ‘Recho’ Ondipo, David Ongano, Elisha Arua na Starford Ochieng.

STUCKING IN THE MIDDLE

Kando na uigizaji dada huyu ni produsa anajivunia kuzalisha filamu kama: ‘Mambo mambo’, ‘Stucking in the middle’, ‘The orphan’, ‘The high way,’ na ‘Vundo series’ chini ya kundi liitwalo Bandilisha Arts Production. Kisura huyu anayejivunia kuwa katika tasnia ya uigizaji kwa miaka minane anadokeza kuwa bado analenga kusaidia wenzake wanaokuja kutambua vipaji vyao na kuwasaidia siku sijazo.

Katika maigizo binti huyu anajivunia kushiriki vipindi tofauti ikiwemo Auntie Boss (NTV), Daktari (KTN), The Real Househelps of Kawangware na Hulabaluu (Maisha Magic East). Anataka mashirika yanayomiliki vyombo vya habari nchini kuanzisha vipindi zaidi kupeperusha filamu zinazozalishwa na wazalendo ili kuwapa ajira wasanii chipukizi.

MCHOYO

Binti huyu kamwe sio mchoyo anashauri wenzake wanaoibukia kuwa wavumilivu na wafanye kazi kwa kujitolea hata wakipata nafasi gani. Anawaambia kuwa kujituma kwao kutachangia watambulike wanatosha mboga katika maigizo. Pia anashauri wasanii chipukizi kuwa endapo wanahisi wana talanta wasisubirie miaka iende mbali muda ndio huu watafute jinsi ya kuingia katika ulingo wa maigizo. Hata hivyo anashikilia kuwa uigizaji siyo mteremko unahitaji nidhamu, kujitolea na kujituma bila kulegeza kamba vile vile pia kumtegemea Mungu zaidi.