Kimataifa

Burundi kukatiza uhusiano wake na Umoja wa Mataifa

June 1st, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

BURUNDI imetisha kukatiza uhusiano wake na balozi wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwaka 2020 ambao serikali inasisitiza ni suala la kindani, mabalozi wa Umoja wa Mataifa walisema.

Jumanne, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililazimika kufutilia mbali mkutano uliopangwa kuhusu Burundi baada ya serikali ya nchi hiyo kutangaza wazi kuwa ilikuwa tayari kusitisha uhusiano na Michel Kafando, mabalozi katika baraza hilo walisema.

Kafando ambaye ni Rais wa zamani wa Burkina Faso, aliteuliwa 2017 kuongoza juhudi za Umoja wa Mataifa nchini Burundi, ambayo ilikuwa imekumbwa na vita kwa zaidi ya mwongo mmoja zilizomalizika 2006.

Ufaransa iliomba baraza liandae mkutano wa faragha kujadili Burundi Ijumaa lakini mazungumzo hayo yaliahirishwa jadi Juni kutoa muda wa kutuliza hali, mabalozi walisema.

Mnamo Alhamisi alipoulizwa kuhusu mzozo wa Burundi na balozi huyo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq alisema: “Sijapata tangazo rasmi kutoka Burundi, kwa hivyo sina la kujibu kwa sasa.”

Burundi imekuwa ikikumbwa na msukosuko tangu Rais Pierre Nkurunziza alipogombea kipindi cha tatu kwenye uchaguzi wa 2015 na kushinda. Upinzani ulisusia uchaguzi huo.

Watu 1200 waliuawa na zaidi ya 400,000 wakatoroka makwao ghasia zilipolipuka nchini humo kati ya Aprili 2015 na kuendelea hadi Mei 2017. Umoja wa Mataifa unasema mauaji yalitekelezwa na maafisa wa usalama wa serikali.

Awashangaza wakosoaji

Mwaka 2018, Nkurunziza alitangaza kuwa hatagombea kwenye uchaguzi mkuu ujao na kushangaza wakosoaji wake waliomlaumu kwa kutaka kukwamilia mamlakani.

Balozi wa Burundi katika Umoja wa Mataifa Albert Shingiro amekuwa akiitaka baraza la usalama kukomesha mikutano inayofanyika kila baada ya miezi mitatu kujadili hali katika nchi yake.

Shingiro anasema kwamba hali nchini Burundi sio tisho kwa usalama na amani ulimwenguni, msimamo ambao unaungwa na Urusi, China na mataifa yanayowakilisha Afrika katika baraza hilo.

Shingiro aliambia AFP: “Burundi haitakubali masuala yake ya ndani kuingiliwa na wageni hata kama hadhi yao ni gani.”

Uhusiano kati ya Umoja wa Mataifa na Burundi umekuwa baridi.

Mnamo Machi, Burundi ilifunga afisi ya shirika hilo kuhusu haki za binadamu jijini Bujumbura.

Kafando alichukua nafasi ya Jamal Benomar, aliyekuwa balozi wa Umoja wa Mataifa kwa miaka miwili kabla ya serikali ya Bujumbura kutaka ajiuzulu.

Vitisho vya Burundi vilijiri miezi minne baada ya Somalia kumfukuza balozi wa Umoja wa Mataifa ambaye alizua maswali kuhusu haki za binadamu katika nchi hiyo.