Michezo

Butterfly FC na MKU Thika zavuna ushindi

March 5th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Gogo Boys ilichezea kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Butterfly FC wakati CMS Allstars ikicharazwa magoli 3-2 na MKU Thika kwenye mechi za Kanda ‘C’ Ligi ya Taifa Daraja ya Pili.

Wanasoka wa Butterly waliokuwa nyumbani katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Githunguri, waliingia mjegoni kwa kusudi moja kutesa na kujiongezea alama zote tatu.

Kikosi hicho kiliwaonyesha wapinzani wao mchezo safi na kuzoa mafanikio hayo kutokana mabao ya Jeremy Nyongesa na Steve Angulu.

Wachana nyavu wa Butterfly chini ya kocha, Bernard Shikuri walitandaza gozi ya chini kwa chini walipania kulipiza kisasi baada ya kupigwa mabao 3-2 na MKU Thika wiki iliyopita.

”Hakika tuna furaha kuvuna ushindi huo lakini bado tuna shughuli zito kwenye kampeni za ngarambe ya msimu huu,” meneja wa Butterfly, Fredrick Ndinya alisema na kuongeza kwamba wanalenga kuendeleza mtindo huo kwenye mechi sijazo.

Nayo Gor Mahia Youth ilidhalilisha Kibera United kwa magoli 5-0 kwenye patashika iliyosakatiwa uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Kwenye mfululizo wa mechi hizo, Bomas of Kenya ilikubali kulala kwa mabao 3-0 mbele ya Wajiji FC, Karatina Homeboys ilitoka sare tasa na Mathaithi huku Gathanga FC ikinasa matokeo sawa na hayo dhidi ya Maafande wa Spitfire FC