Michezo

Butterfly FC yaangushia MKU Thika makombora mawili

May 21st, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya MKU Thika ilichabangwa mabao 2-0 na Butterfly FC huku Gor Mahia Youth na Tandaza FC kila moja ikiyeyusha alama mbili kwenye mechi za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu huu.

Gor Mahia Youth na Tandaza zilitoshana nguvu mabao 3-3 na 2-2 mbele ya Gathanga FC na Maafande wa Spitfire mtawalia.

Gor Mahia Youth na wapinzani wao ziliteremsha soka safi ambapo Gor Mahia Youth ilifaulu kupata mabao hayo kupitia Eliud Lukuwuom, Lyodd Kavuchi na Josephat Lopagat.

Butterfly FC ya kocha, Bernard Shikuri ilivuna ushindi huo na kulipiza kisasi baada ya kulazwa mabao 2-1 na Bomas of Kenya wiki iliyopita.

”Katika mpango mzima tungali mbioni kusaka ubingwa wa taji la msimu huu ingawa tunakubana na upinzani mkali kwenye kampeni za msimu huu,” kocha wa Butterfly alisema na kushukuru vijana wake kwa ufanisi huo.

Butterfly imerukia nafasi ya pili kwenye jewdali kwa kukusanya pointi 38, moja mbele ya Tandaza FC. Nayo Gor Mahia Youth ingali kileleni kwa kuvuna alama 45.

Naye Noah Wafula alifunga bao moja tamu na kubeba CMS Allstars kukomoa Bomas of Kenya bao 1-0, wakati Kibra United iliagana sare ya bao 1-1 na Gogo Boys.