Michezo

Butterfly kusajili wawili kujisuka upya

April 14th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

BUTTERFLY FC inalenga kutwaa huduma za wachezaji wawili wapya kujiweka imara kukabili wapinzani wao kwenye michuano ya mkumbo wa pili kwenye kampeni za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu huu.

Mshirikishi wa Butterfly, Daniel Obura anasema ”Tunalenga kusaka wachezaji wawili wapya maana tumegundua kwamba kampeni za msimu huu kamwe siyo mteremko timu zote zimejipanga kitifua vumbi kali kupigania tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki ngarambe ya Supa Ligi ya Taifa (NSL) msimu ujao.”

Ofisa huyo anasema wamepania kuongezea safu ya mbele nguvu ili kufunga mabao yatakayowawezesha kufanya kweli msimu huu.

Aidha anadokeza kwamba bado wana imani wanaweza kufanya vizuri licha ya ushindani mkali unaoshuhudiwa kwenye kampeni za msimu huu. Butterfly ni kati ya vikosi vinavyopigiwa chapuo kutesa kwenye kampeni za kipute hicho msimu huu.

Butterfly FC ya kocha, Bernard Shikuri ilikamilisha mechi za mkumbo wa kwanza ikiwa katika nafasi ya pili kwa kuzoa alama 26 sawa na Tandaza FC tofauti ikiwa idadi ya mabao. Kwenye msimamo wa Kundi hilo, Gor Mahia Youth inaendelea kuongoza baada ya kufikisha alama 32.

Msimu uliyopita Butterfly FC ilikuwa miongoni mwa vikosi vilivyotisha wapinzani wengine kwneye kampeni za kipute hicho kabla ya kuteleza na kumaliza ya pili kwenye jedwali ikifuata Buruburu Sports iliyopandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Kwanza msimu huu.

Butterfly inajivunia wachezaji wepesi akiwamo Ben Wande, Wanjala Mwarabu, Duncan Makaya, Teddy Otieno na Stephen Angulu mfungaji wa kikosi hicho.