Michezo

Butterfly, Tandaza na Gor Mahia Youth kusaka ushindi wikendi

April 4th, 2019 1 min read

NA JOHN KIMWERE

BUTTERFLY FC, Tandaza FC na Gor Mahia Youth wikendi hii zimeratibiwa kuingia uwanjani kusaka alama tatu muhimu huku zikikamilisha mkondo wa kwanza wa mechi za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili.

Butterfly FC ya kocha Bernard Shikuri Jumapili itakuwa ugenini kukabili Kibra United Uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Nayo Tandaza FC inayoshikilia nafasi ya pili itakuwa katika ardhi ya nyumbani Lower Kabete kukaribisha Wajiji FC kwenye mechi itakapokuwa mbioni kupigania alama zote ili kuendelea kusonga mbele kwenye jedwali.

Gor Mahia Youth inayoongoza kipute hicho itaalika Mathaithi FC katika Uwanja wa Camp Toyoyo Jericho Nairobi.

Butterfly itashuka dimbani ikilenga pointi tatu baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 na Gathanga FC wiki iliyopita.

“Katika mpango mzima tutakuwa mbioni kuwinda alama zote ili kujiongezea tumaini la kusonga mbele pia tufunge mkondo wa kwanza vyema,” meneja wa Butterfly alisema na kuongeza kwamba kipute cha mwaka huu kinazidi kuzua ushindani mkali kinyume na ilivyotarajiwa.

Kwenye mfululizo huo, Gogo Boys itakutanishwa na Bomas of Kenya Jumamosi uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Nayo Karatina Homeboys Jumamosi itazuru jijini Nairobi kucheza na Maafande wa Spitfire FC Uwanjani Moi Air Base.