Michezo

Butterfly washindwa kupepea Tandaza ikiwakung'uta CMS Allstars

April 2nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

BUTTERFLY FC iliteleza na kuyeyusha alama mbili muhimu wakati Tandaza FC ikituzwa pointi tatu bila jasho ikiwa ni ushindi wa mezani kwenye mechi za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu huu.

Matumaini ya Butterfly FC kujiongezea alama zote yaligonga mwamba ilipolazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Gathanga FC kwenye mchezo uliyopigiwa Uwanja wa Shule ya Msingi ya Githunguri. Ben Wande aliiweka Butterfly kifua mbele kabla Gathanga kusawazisha kipindi cha pili.

Nayo Tandaza ilitwaa pointi tatu bila jasho baada ya wapinzani wao CMS Allstars kushindwa kuleta maafisa wa kulinda usalama Uwanjani.

”Ndivyo ilivyo hatuna budi ila tulikubali yaishe,” meneja wa Butterfly Fredrick Ndinya alisema na kuongeza kwamba lazima wachezaji wake wakaze buti maana kampeni za msimu huu siyo mteremko.

Nayo Gor Mahia Youth iliichapa Karatina Homeboys bao 1-0 na kuendelea kukaa kifua mbele kwenye msimamo wa kipute hicho kwa alama 26.

Nayo Tandaza inafunga mbili bora kwa alama 23, mbili mbele ya Butterfly FC. Naye Hillary Shirao alipiga ‘Hat trick’ na kubeba Gogo Boys kukandamiza Mathaithi FC kwa mabao 3-1.

Mathaithi ilijipatia bao la kufuta machozi kupitia juhudi zake Francis Maina kwenye patashika hiyo iliyopigiwa Karatina stadium mjini humo.