Michezo

Butterfly yaigonga Mathare Gor Mahia Youth ikitoka sare

June 25th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

DAVIS Nyangeres alipiga kombora moja safi na kubeba Butterfly FC kubugiza Kibera United bao 1-0 wakati Gor Mahia Youth ikitoka sare ya bao 1-1 na Mathaithi FC uwanjani Karatina Stadium mjini humo.

Nayo Tandaza FC ilidondosha alama mbili muhimu na kubanduliwa katika nafasi ya pili ilipolazwa bao 1-0 na Wajiji FC kwenye patashika iliyopigiwa katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Tumaini, Embakasi Nairobi.

Matokeo hayo yamefanya Butterfy FC kujiongezea tumaini la kumaliza mbili bora endapo itafanya kweli kwenye mchezo wa mwisho. ”Nashukuru vijana wangu kwa kujitahidi na kufanikiwa kuhimili makali ya wageni wetu na kuzoa pointi tatu muhimu,” meneja wa Butterfly, Fredrick Ndinya alisema.

Kwenye matokeo hayo, Bomas of Kenya ilijipatia pointi moja baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Gogo Boys. Nevile Ochieng alifungia Bomas of Kenya nayo Gogo Boys ilisawazisha kupitia Ramadhan Adati Abdulltif.

Kadhalika matumaini ya Maafande wa Spitfire FC kunasa pointi zote yaliogonga mwamba ilipotoka nguvu sawa bao 1-1 na Karatina Homeboys.

Kwenye jedwali ya kipute hicho, Gor Mahia Youth ingali kifua mbele kwa kuvuna pointi 54, saba mbele ya Butterfly FC huku Tandaza FC ikifunga tatu bora kwa alama 44, moja mbele ya CMS Allstars iliyotoka sare ya bao 1-1 na Gathanga FC.