Michezo

Butterfly, Gor Mahia Youth na Tandaza FC ushindi tu

April 8th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WANASOKA wa Butterfly FC, Gor Mahia Youth na Tandaza FC wanazidi kutifua vumbi kwenye mechi za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu huu.

Gor Mahia Youth na Butterfly FC kila moja ilijiongezea alama tatu muhimu huku Tandaza FC ikituzwa ushindi wa mezani na kuendelea kukaa bega kwa bega.

Mfungaji shupavu alicheka na wavu mara mbili naye Teddy Otieno alitinga bao moja na kusaidia Butterfly kuchoma Kibra United kwa mabao 3-0 kwenye patashika iliyochezewa Uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Nao limbukeni wa Gor Mahia Youth waliizima Mathaithi FC kwa mabao 3-0 wakati Tandaza FC ikisajili alama zote muhimu bila jasho baada ya wapinzani wao Wajiji FC kuingia mitini.

Baadhi ya wachezaji wa akiba wa Gor Mahia Youth wakifuatilia wenzao wakicheza na Butterfly kwenye mechi Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili uwanjani City Stadium, Nairobi. Gor Mahia Youth ilishinda mabao 3-2. Picha/ John Kimwere

Butterfly ya kocha, Bernard Shikuri ilishuka dimbani kwa kusudio moja kutesa na kubeba pointi zote baada ya kutoshana nguvu bao 1-1 na Gathanga FC wiki iliyopita.

”Hakika tuna kazi zito lazima tujikaze ili kuwapiku wapinzani wetu,” meneja wa Butterfly FC, Fredrick Ndinya alisema na kuongeza hakuna kupumziko.

Kwenye jedwali ya kipute hicho, Gor Mahia ingali kifua mbele kwa alama 32, Tandaza FC ya pili kwa kuzoa pointi 26 sawa na Butterfly tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Kwenye mfululizo wa michezo hiyo, Bomas of Kenya ya kocha, David Dinda ilitoka sare tasa na Gogo Boys, naye Collins Mwanzi alitikisa wavu mara moja na kubeba CMS Allstars kuifunga Gathanga FC kwa bao 1-0.

Masaibu ya Karatina Homeboys yaligeuka faida kwa Maafande wa Spitfire iliyotuzwa pointi tatu kiulaini, Karatina Homeboys iliachia alama zote iliposhindwa kufika Uwanjani Moi Airbase, Nairobi kuvaana na Maafande wa Spitfire.