Kanini Kega abadili kauli ya kumuunga Raila 2022, asema ‘Gideon Moi tosha’

Kanini Kega abadili kauli ya kumuunga Raila 2022, asema ‘Gideon Moi tosha’

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kieni Bw Kanini Kega ameonekana kubadilisha kauli yake ya kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Bw Kega alikuwa miongoni mwa wabunge na wanasiasa kutoka eneo la Kati chini ya vuguvugu la Kieleweke, walioandamana na Bw Odinga na kuahidi kumuunga mkono 2022 wiki iliyopita.

 

Alhamisi katika kongamano la Kanu ambapo chama hicho kilimteua kiongozi wake, Bw Gedion Moi kupeperusha bendera ya urais uchaguzi mkuu ujao, Bw Kega alionekana kubadilisha ahadi yake kwa Raila.

“Bw Gideon Moi una vigezo vyote vinavyohitajika kuwa rais mwaka ujao. Ninakuunga mkono,” Kega akasema.

Mbunge huyo aidha alisema alipata mwaliko kuhudhuria kongamano hilo la wajumbe wa Kanu, kupitia Bw Gedion Moi ambaye pia ni seneta wa Baringo na aliyemtaja kuwa “sahibu”.

“Aliponipigia simu, niliwasiliana na bosi wangu ambaye pia ni bosi wenu, Rais Uhuru Kenyatta akanipa ruhusa kuhudhuria,” Bw Kega akadokeza, akihutubia wajumbe.

Bw Odinga, Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetangula (Ford-Kenya), na Isaac Ruto (Chama Cha Mashinani) ni kati ya wageni mashuhuri waliohudhuria hafla hiyo ya Kanu.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, KANU ilitia saini mkataba wa makubaliano kushirikiana na chama tawala cha Jubilee.

You can share this post!

KANU yamteua Gideon Moi kuwania urais 2022

Kalonzo awalilia vinara wa OKA wampe tiketi apeperushe...