Kimataifa

Bwana harusi akata tamaa ya kuishi baada ya mlipuko kuwaua 63 kwenye sherehe yake

August 19th, 2019 1 min read

NA AFP

BWANA harusi ambaye sherehe yake ilikatizwa na mlipuaji wa kujitoa mhanga mjini Kabul, amesema amepoteza matumaini ya kuendelea kuishi baada ya kisa hicho cha maangamizi siku ya Jumapili.

Mirwais Elmi alisema anakumbuka jinsi hafla hiyo ilivyojaa shamrashamra nyingi, lakini baada ya muda mfupi mazingira yakabadilika na miili ya waliokuja kushuhudia ndoa yake ikatapakaa ukumbini, wengine wakiwa na majeraha na wengine wakiwa wafu.

Ingawa mpenziwe alinusurika, nduguye pamoja na jamaa zake wengine walikuwa kati ya watu 63 ambao walifariki baada ya mlipuaji wa kujitolea mhanga kushiriki kitendo hicho cha kigaidi.

“Familia yangu, mpenzi wangu bado wametamauka na hata hawawezi kuzungumza. Mpenzi wangu amekuwa akizirai na kupoteza fahamu kila mara. Nimekata tamaa. Nimepoteza ndugu zangu, marafiki na jamaa. Sitawahi kuonja furaha tena maishani mwangu,” akasema Elmi.

Aliongeza kuwa hawezi kuhudhuria mazishi ya walioaga dunia kwa kuwa amekuwa mnyonge sana.

Elmi alisema matukio kama hayo yataendelea kushuhudiwa Afghanistan pasipo mikakati tosha ya kiusalama.

Kundi la kigaidi la ISIS limekiri kuhusika na shambulizi hilo ambalo pia liwaacha watu 182 na majeraha mabaya.