Kimataifa

Bwana harusi mwoga wa radi afanya kidosho akatishe harusi

July 11th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

BIHAR, INDIA

SHEREHE ya harusi ilikatizwa ghafla baada ya bwana harusi kuogopeshwa na mwale wa radi katika kijiji cha Chitrasenpur, India.

Ripoti zinasema hofu kubwa ya bwana harusi ilimfanya mchumba wake afutilie mbali harusi hiyo, na kukatokea vita kwani familia ya bwana harusi haikupendezwa na hatua hiyo.

Jamii ya bwana harusi ililalamika kuwa matambiko ya harusi yalikuwa tayari yashafanywa na haikufaa hafla hiyo isitishwe mahali ilipofikia.

Polisi waliokuja kutuliza ghasia zilizoibuka walinukuliwa kusema bibi harusi aliondoka harusini kwa hasira kwa kuwa hakufurahishwa na uoga wa mwanamume huyo ambao si wa kawaida.

Kulingana na mashirika yahabari, jamii ya bibi harusi ndiyo ilizua rabsha wakati ile ya bwana harusi ilipolalamikia uamuzi wa mwanamke huyo.

Kwa mujibu wa polisi wa eneo hilo, jamaa watatu wa upande wa bibi harusi walikamatwa baada ya mapigani hayo.

Haikubainika wazi kama kuna yeyote aliyejeruhiwa.

-Imekusanywa na Valentine Obara