Habari Mseto

Bwanyenye aliyetoweka Septemba ajitokeza

December 8th, 2020 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

BWANYENYE wa mji wa Thika aliyetoweka wiki 11 zilizopita amerejea nyumbani huku akisema kuwa aliachiliwa huru na watu waliokuwa wamemteka nyara.

Bw Julius Gitau, maarufu Gitau wa Mali, aliambia polisi kuwa watu waliomteka nyara walimwachilia huru Jumamosi katika eneo ambalo baadaye aligundua kwamba ilikuwa Kamwangi, eneobunge la Gatundu Kaskazini.

Baada ya kuachiliwa, Bw Gitau alielekea nyumbani kwa mkewe wa tatu, Bi Selina Nelly ambaye ni afisa wa polisi mjini Thika.

Maafisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) walisema kuwa walinasa mawimbi ya simu ya Bw Gitau alipokuwa akiongea na mkewe.

Walimfuata na kumpata akiwa nyumbani kwa mkewe wa tatu na kumtaka kuripoti katika afisi za DCI za Gatanga.

Milionea huyo aliambia polisi kuwa alitekwa nyara na watu waliokuwa na bunduki karibu na afisi za Mamlaka ya Ushuru (KRA) tawi la Thika mnamo Septemba 21 asubuhi.

Alisema kuwa alitekwa alipokuwa akielekea katika jumba la mazoezi ya viungo (gym) na akapoteza fahamu baada ya watu hao kumlazimisha kunywa soda.

Bwanyenye huyo alisema alijipata ndani ya jumba kubwa ambamo alifichwa kwa wiki 11.

“Nilikuwa nikilazimishwa kufua nguo na kuosha vyombo vinavyotumiwa na wapangaji katika jumba hilo,” akasema Bw Gitau.

Aliambia polisi kuwa hakupata fursa ya kutambua mmiliki wa jumba hilo na wala hawezi kutambua lipo eneo gani nchini Kenya.

Polisi wa Murang’a waliohojiwa na Taifa Leo, hata hivyo walisema kuwa maelezo ya mfanyabiashara huyo hayaaminiki.

Walisema kuwa watatumia teknolojia na wataalamu mbalimbali kutathmini ukweli wa maelezo ya mfanyabiashara huyo.