Habari Mseto

Bwanyenye wa Zimbabwe ashangaza alivyopanga maziko yake kabla ya mauti

November 11th, 2020 2 min read

MASHIRIKA NA WANGU KANURI

BWANYENYE mtajika nchini Zimbabwe Genius Kadungure almaarufu Ginimbi ameshangaza wengi baada ya kuibuka kuwa alikuwa amenunua jeneza wiki moja kabla ya ajali iliyoyakatisha maisha yake kufanyika.

Isitoshe, dadake marehemu, Juliet Kadungure amefichua kuwa kakake alikuwa amepanga jinsi mazishi yake yatakavyoendeshwa mwezi mmoja kabla ya kufa kwake huku akiwa na orodha kamili ya watakaohudhuria, wageni waheshimiwa na mavazi yatakayovaliwa na kila mtu atakayehudhuria.

Kulingana na ombi la Ginimbi, kila mtu atakayehudhuria kwenye mazishi yake sharti avalie mavazi meupe. Mavazi hayo yamenasibishwa na jinsi Ginimbi alivyovalia alipokuwa kwenye sherehe zake.

Vile vile, Juliet aliongeza kwa kusema kuwa kulingana na utaratibu ambao marehemu Ginimbi alikuwa amewacha, marafiki zake ambao wanaishi barani Afrika sharti wawepo kwenye mazishi na kama watachelewa basi mazishi yaahirishwe.

Alizidisha kwa kusema kuwa marehemu alitaka asizikwe kwa haraka. Hali kadhalika, marehemu Ginimbi alitaka jumba lake kifahari lifanywe hoteli ama jumba la makumbusho atakapoaga.

Imeripotiwa kuwa Ginimbi alikuwa akiliendesha gari lake aina ya Rolls Royce Wraith kwa kasi alipogongana na gari aina ya Honda Fit.

Gari lake Ginimbi liliondoka barabarani na kugonga mti ambapo liliteketea kadiri ya kufahamika huku likimuua pamoja na waabiri wenzake ambao ni Mimie Moana, rafikiye wa kike wa Moana Elisha na rafikiye Ginimbi, Limumba Karim. Watatu hao waliteketea kadiri ya kujulikana huku mwili wa Ginimbi ukiwa na majeraha ya moto.

Ginimbi alikuwa akitoka katika sherehe ya kuzaliwa kwa Michelle Amuli almaarufu Mimie Moana katika klabu mojawapo mjini Harare ya Dreams.

Saa chache kabla ya mwendazake kuondoka nyumbani kwake na kuelekea katika klabu hiyo ya Dreams, aliwarekodia video wafuasi wake akiwafahamisha kule atakakokuwa kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram.

“Ni wakati wa kutoka. Tunaenda klabu ya Dreams baada ya dakika chache zijazo ambako kutakuwa na sherehe. Tutakuwa tukisherehekea siku ya kuzaliwa kwake Moana na tutazifungua mvinyo kadhaa. Tuonane huko,” alisema.

Mwendazake Genius Kadungure alikuwa amevutiwa sana na biashara ya petroli na gesi na hadi kifo chake alikuwa mwanabiashara tajika mwenye kampuni ya uuzaji wa gesi nchini na hata nchi jirani.

Alifahamika na wengi kwa vile alivyoishi na alivyokuwa na magari ya kifahari aina nyingi ambayo ni Bentley Continental, Ferrari, Rolls Royce Ghost, Lamborghini Aventador S Roadster, Rolls Royce Wraith, Range Rovers, Mercedes Benz S Class na BMW.

Marehemu Ginimbi atazikwa Novemba 14, 2020 katika shamba lake kama alivyotaka.