Makala

Bwawa hatari kwa wakazi Nyeri

September 15th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Barabara inayounganisha mji wa Nyeri na Karatina ni yenye shughuli chungu nzima za usafiri na uchukuzi, ikizingatiwa kuwa Kaunti ya Nyeri ni maarufu katika kilimo.

Kimsingi, kila dakika ni barabara isiyokosa magari ikikumbukwa kuwa pia ndiyo inaunganisha kaunti ya Laikipia, Meru, Isiolo, Kirinyaga, Murang’a na Nairobi.

Pembezoni mwa barabara hiyo, kati ya Ngandu na Marua, lipo bwawa ambalo kulingana na wakazi athari zake zimepiku faida.

Bwawa hilo maarufu kama ‘Demu’ limekuwepo kwa muda wa miaka mingi, kizazi kilichopo kikidai walilipata humo.

Linapotajwa, linafufua makovu ya kidonda cha Keziah Wanjiru. Miaka tisa iliyopita, alipoteza mumewe kupitia bwawa hilo.

“Alikuwa mhudumu wa bodaboda na 2010 baada ya pikipiki yake kupoteza mwelekeo, ilitumbukia humo. Ilichukua muda wa siku kadhaa kuuopoa mwili wake,” Keziah anasimulia, tukio ambalo anasema lilibadilisha mkondo wake wa maisha kuwa wenye majonzi.

Kulingana na mama huyo mchanga, wakati wa mkasa huo walikuwa wamejaliwa mapacha, mwaka mmoja uliotangulia.

Mjane huyo anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba baada ya kupoteza kibarafu chake cha moyo, alianza kupitia unyanyapaa katika familia aliyooleka.

Wakazi wanalalamikia kwamba limechangia kukithiri kwa visa vya uhalifu. Kabla chuma nguzo ya barabara kuwekwa, magari na pikipiki, yalikuwa yakitumbukia humo na kusababisha maafa. PICHA/ SAMMY WAWERU

“Hatimaye nilifurushwa boma hilo, nikaanza maisha upya na wanangu wachanga. Haikuwa rahisi. Hata hivyo, Mungu alinifungulia milango ya heri, nikajaaliwa kazi Nairobi,” Keziah akasema.

Miaka kadhaa iliyopita, gari lililokuwa na idadi ya watu isiyojulikana lilitumbukia katika bwawa hilo hilo. David Karira, mkazi wa Thaithi, anasema hicho si kisa cha kwanza kushuhudiwa. Wakati wa mahojiano, alisema kabla ya chuma nguzo ya barabara kuwekwa na serikali visa vya magari kutumbukia humo vilikuwa vinashuhudiwa mara kwa mara.

Cha kushangaza ni kwamba kati ya Ngandu na Thaithi, barabara haina matuta kupunguza kasi ya magari. Kando na kuwa hatari kwa magari, David alisema bwawa hilo limechangia kuongezeka kwa visa vya uhalifu.

“Usiku wahuni huhangaisha wanaofika wakiwa wamechelewa kwa kuwapora, kuwapiga na hata kuwarusha kwenye bwawa,” akalalamika.

“Barabara yenyewe haina mataa ya usalama, tumepoteza wenyeji waliovamiwa na wahalifu,” akaongeza Purity Kariuki, mkazi. Isitoshe, ukosefu wa matuta eneo hilo kulingana na Purity umechangia kuwepo kwa visa vya ajali.

Hata ingawa wakazi wanasema bwawa hilo limesaidia kuimarisha shughuli za kilimo, ambapo hutumia maji yake kukuza mazao, wanaomba serikali kulizingura kwa nyaya na vyuma na pia kuimarisha usalama.

La sivyo, wanasema litaendelea kuwanyima amani kutokana na hatari ambayo bwawa hilo linaibua.