Habari

BWAWA LA MAUTI: Watu 44 waangaamia kwenye mkasa Nakuru

May 10th, 2018 3 min read

MAGDALENE WANJA na ERIC MATARA

Kwa Muhtasari:

  • Wakazi walisikia mlipuko mkubwa kabla ya maji kusomba nyumba zao pamoja na makazi 
  • Baada ya kuvunja kingo zake, maji ya bwala hilo yalifyatuka kwa kasi kwa sababu bwala hilo liko katika nyanda za juu huku wakazi wakiwa wamejenga maeneo ya chini ya bwala hilo
  • Shirika la Msalaba Mwekundu walithibitisha kupata miili ya watu 44 huku zaidi ya waathiriwa 40 wakiendelea kupata matibabu katika hospitali za Bahati na Nakuru Level 5
  • Takriban maafisa 200 wa KDF waliwasili eneo hilo wakitumia ndege za kijeshi ili kuwasaidia maafisa wa Msalaba Mwekundu na wale wa Kaunti ya Nakuru

WATU wapatao 44 walipoteza maisha yao Jumatano usiku baada ya Bwala la Patel lililoko eneo la Solai, Kaunti ya Nakuru kuvunja kingo zake na kusomba vijiji viwili. Idara tofauti zilitoa takwimu zilizokinzana kuhusu idadi kamili ya vifo.

Kisa hicho kilichotokea mwendo wa saa moja jioni kiliongeza idadi ya vifo vilivyotokana na mvua nchini mwaka huu hadi 150 huku zaidi ya watu 300,000 wakikosa makao.

Maafisa wa Msalaba Mwekundu wanakili data kwenye Hospitali ya Nakuru Level Five kufuatia mkasa wa Solai. Picha/ Ayub Muiyuro

Wakazi wa Solai waliambia Taifa Leo kuwa walisikia mlipuko mkubwa kabla ya maji kusomba nyumba zao pamoja na makazi katika shamba kubwa la Nyakinyua.

Mkuu wa Polisi eneo Rongai, Japheth Kioko alisema bado kuna idadi kubwa ya watu ambao bado hawakuwa wamepatikana.

“Tulipata miili 11 ikiwa imefunikwa na matope katika shamba la kahawa na tunashuku miili hiyo ni ya watu waliokuwa wanajaribu kutoroka lakini wakashindwa nguvu na maji,” alisema Bw Kioko.

Maafisa wapakia kwenye gari mwili wa mmoja wa wakazi waliongamia kwenye mkasa. Picha/ Ayub Muiyuro

Alisema wengi wa waliopoteza maisha ni akina mama na watoto ambao walikuwa manyumbani jioni.

Tukichapisha habari hii, maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu walithibitisha kupata miili ya watu 33 huku zaidi ya waathiriwa 40 wakiendelea kupata matibabu katika hospitali za Bahati na Nakuru Level 5.

Mary Karimi, mmoja wa waathiriwa, alisema bado anawatafuta watoto wake, akiwemo mmoja wa miaka minne.

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i azifariji familia ambazo zilizopoteza jamaa wao kwenye mkasa wa Solai Mei 10, 2018. Picha/ Ayub Muiyuro

“Wakati tuliposikia sauti kubwa tulidhani ni mvua kubwa inanyesha. Tulikuwa tumechanganyikiwa. Natumai watoto wangu wako hai,” alisema Bi Karimi kwa majonzi.

Pius Mzee alikuwa anapiga gumzo na mkewe pamoja na watoto wake wanne nyumbani wakati maji yalipovamia nyumba yao. Alisema alijaribu kutoroka na binti zake wawili wenye umri wa miaka nne na sita lakini akalemewa. Baada ya maji kumshinda nguvu, Mzee aliachilia watoto wake na kupanda juu ya mti.

 

‘Sijui familia yangu iliko’

“Mke wangu alikuwa ameshikilia watoto wawili na punde baada ya maji kuongeza kasi sikujua walielekea wapi. Kufikia sasa sijui wako wapi,” alielezea Mzee akiwa hospitalini Nakuru Level Five anakoendelea kupata matibabu.

Wakazi waonyesha pahali mkasa wa bwawa la Patel ulianzia. Picha/ Ayub Muiyuro

Naye James Njung’e, ambaye pia anaendelea kutibiwa, alisema maji hayo yalimpata nyumbani akiwa na wazazi na mpwa wake.

“Tulisikia mlipuko mkubwa ambao tulidhani ni mvua. Punde maji yalivunja mlango na kuingia kwa kasi,” alielezea Njung’e.

Kwa bahati nzuri, Njung’e na jamaa wake waliponea baada ya kujishikilia kwenye mabaki ya nyumba.

George Wanjala mwenye umri wa miaka 25, alisema alipoteza watoto wake watatu akiwemo mmoja wa miezi miwili. Waathiriwa 13 walitibiwa Alhamisi na kuruhusiwa waende nyumbani.

Mashine hii inajaribu kuondoa matope yaliyosababishwa na maji kutoka kwa bwawa la Solai ililovunja kingo zake Mei 9, 2018. Picha/ Jeff Angote

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet na Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui waliongoza vikosi vya uokoaji katika eneo hilo huku wakazi wa maeneo jirani ya Marigu, Ruiru na Akuisi wakitoroka makwao kwa hofu ya mafuriko zaidi.

“Hatuna muda wa kupoteza. Serikali kuu inashirikiana kwa karibu na serikali ya Kaunti ya Nakuru ili kusaidia familia zilizoathirika,” alisema Dkt Matiangi.
Waziri Matiang’i alisema serikali imetoa vyandarua kwa walioathirika pamoja na chakula cha msaada.

 

Msaada wa KDF

Takriban maafisa 200 wa KDF waliwasili eneo hilo wakitumia ndege za kijeshi ili kuwasaidia maafisa wa Msalaba Mwekundu na wale wa Kaunti ya Nakuru.

Maafisa wa Msalaba Mwekundu walisema kuta za bwawa hilo zilishindwa nguvu na maji yaliyokuwa yanaongezeka kwa wingi kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na kuvunja kingo zake kisha kufyeka zaidi ya familia 300.

Baadhi ya vyombo ambayo waakzi walifanikiwa kuokoa katika mkasa huo. Picha/ Jeff Angote

Bwawa hilo kubwa liko katika shamba kubwa la mkulima maarufu Mansukul Patel eneo la Solai.

Baada ya kuvunja kingo zake, maji ya bwala hilo yalifyatuka kwa kasi kwa sababu bwala hilo liko katika nyanda za juu huku wakazi wakiwa wamejenga maeneo ya chini ya bwala hilo.

Gavana Kinyanjui alisema watachunguza iwapo Bw Patel alikuwa na leseni ya kujenga bwawa katika nyanda za juu.

Makazi yalivyoharibiwa na maji hayo. Picha/ Jeff Angote

Tukichapisha habari hii, zaidi ya watu 50 walikuwa wameokolewa lakini juhudi za uokoaji zikasitishwa kutokana na giza.

Gavana Kinyanjui alisema serikali ya kaunti imefungua kituo cha kutoa habari kuhusu walioathiriwa katika afisi ya Naibu wa Kamishna wa Kaunti eneo la Solai.

Iliwalazimu maafisa wa Kenya Power kuzima stima eneo lote baada ya vikingi vya stima kusombwa na maji.