Habari

Bweni lateketea tena shuleni Musingu

November 9th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

BWENI mojawapo katika Shule ya Musingu, kaunti ndogo ya Ikolomani katika Kaunti ya Kakamega limeteketea Jumamosi asubuhi, mali na vifaa muhimu vya wanafunzi vikiteketea.

Watahiniwa 354 walikuwa shuleni mkasa huo ulipotokea.

Hakuna aliyeripotiwa kuangamia.

Kamanda wa Polisi wa Kakamega Kusini Joseph Chesire amesema moto umeanzia katika sehemu ya dirisha ambapo shughuli ya uchomeleaji ilikuwa ikiendelea ikiwa ni njia mojawapo ya kuhakikisha mali ya wanafunzi wengine walio nyumbani kwa likizo inakuwa salama. Ni mkasa badala yake ndiyo umeshuhudiwa.

“Mafundi wawili wa uchomeleaji wamepata majeraha kiasi ambapo wamepelekwa hospitalini Shibwe,” amesema Bw Chesire.

Hata hivyo, uchunguzi unasubiriwa kufanyika ndipo chanzo halisi cha moto kijulikane.

Rasi – mwalimu mkuu – Bw Bernard Lukuya amethibitisha kutokea kwa mkasa huo na kubainisha kwamba watahiniwa wote shuleni hapo wako katika mazingira salama na hivyo katika hali nzuri kuendelea kufanya mtihani wao wa kitaifa wa kidato cha nne.

“Tunasubiri uchunguzi ufanywe kubainisha chanzo hasa cha moto huo. Bweni hilo la Madaraka – Taifa hutumiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza, cha pili na cha tatu ambao kwa sasa wako nyumbani kwa likizo,” amesema Bw Lukuya.

Aliyekuwa Seneta wa Kaunti ya Kakamega Dkt Boni Khalwale amefika shuleni humo ambapo ametaka uchunguzi wa kina ufanywe.

“Hii shule imekuwepo tangu mwaka 1965 na hakujakuwa na mikasa ya moto kama inayoshuhudiwa sasa. Kipindi cha miezi miwili na tayari kuna visa viwili vya moto katika mabweni. Lazima kuna kitu hakiendi sawa,” amesema Bw Khalwale.

Ameutaka usimamizi wa shule hiyo kuita mkandarasi kuchunguza mfumo wa umeme katika bweni jipya la Oparanya kuhakikisha hakuna makosa yanayoweza kusababisha hitilafu za umeme kiholela.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kakamega katika Bunge la Kitaifa Bi Elsie Muhanda amewataka viongozi wajitokeze ili kuwasaidia wanafunzi walioathirika ili wasitaabike shule zitakapofunguka Januari 2020.

Mnamo Septemba 2019 moto uliteketeza bweni katika shule hiyo ya Musingu.