Habari za Kitaifa

Bweni lateketezwa, shule yafungwa mwalimu mkuu akizozana na maafisa wa Kuppet Kitui


SHULE ya Upili ya Wavulana ya Kisasi  Kaunti ya Kitui imefungwa kwa muda usiojulikana baada ya wanafunzi kuchoma bweni huku mgomo wa walimu ukiendelea nchini.

Tukio hilo la Jumapili lilijiri saa chache baada ya Mwalimu Mkuu Francis Muthusi kufarakana na maafisa wa Muungano wa Walimu wa Shule za Upili Nchini na Vyuo vya Kadri (KUPPET) huku wanafunzi wakitazama.

Wanachama wa Kuppet tawi la Kitui walikuwa wamefika shuleni humo kukutana na wanachama wao lakini wakatimuliwa na polisi kutokana na amri ya Bw Muthusi aliyedai walikuwa wamefika kutatiza shughuli za masomo.

Katibu wa Kuppet tawi la Kitui, Benjamin Mutia alimkashifu vikali mwalimu mkuu kwa kudai kuwa maafisa wa Kuppet walikuwa wakilenga kuvuruga shughuli za masomo shuleni humo.

“Mwalimu Mkuu anadai kuwa ziara yetu ilikuwa ya kuvuruga shughuli shuleni humo na akatufukuza. Tulikuwa tumekuja kuzungumza na wanachama wetu ambao alikuwa amewatisha ili wasishiriki mgomo,” akasema Bw Mutia.

Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha moto huo na iwapo unahusiana na ziara ya maafisa wa Kuppet.

Mwalimu Mkuu alithibitisha kuwa wanafunzi wote walikuwa wametumwa nyumbani na akakanusha kuwa kuteketezwa kwa bweni hilo kulitokana na ziara ya maafisa wa Kuppet shuleni humo.

Kuteketezwa kwa bweni hilo Jumapili kulisababisha shule kadhaa kuwarejesha wanafunzi nyumbani, usimamizi ukisingizia kuwa wanatumwa kuleta masalio ya karo.

Mmoja wa walimu wakuu ambaye hakutaka anukuliwe ili kuepuka adhabu ya wizara ya elimu, alisema kuwa kuhakikisha usalama wa wanafunzi shuleni bila walimu ilikuwa changamoto kubwa.

Mkurugenzi wa Elimu Kaunti ya Kitui Khalif Hassan alisema shughuli za masomo zilikuwa zikiendelea kama kawaida katika shule zote kaunti hiyo.

Alikiri kuwa anafahamu baadhi ya wanafunzi walitumwa nyumbani kwa sababu ya kutolipa karo na akasema wanatakiwa kurejea shuleni bila kukawia.