Michezo

Caballero kuendelea kupangua mashuti Stamford Bridge

June 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPA Willy Caballero amerefusha muda wa kuhudumu kwake uwanjani Stamford Bridge baada ya Chelsea kumpa mkataba mpya wa mwaka mmoja zaidi.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 38 ni mzawa wa Argentina. Alitarajiwa kukatiza rasmi uhusiano wake na Chelsea mwishoni mwa muhula huu baada ya kandarasi yake kutamatika Juni 30, 2020.

Hadi kampeni za msimu huu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zilipositishwa kwa muda mnamo Machi kutokana na janga la corona, Caballero alikuwa amewajibishwa na Chelsea katika mechi tisa za ligi.

Mechi tano kati ya hizo zilikuwa zile zilizosakatwa mnamo Februari 2020 baada ya kipa chaguo la kwanza la Chelsea, Kepa Arrizabalaga kutemwa na kocha Frank Lampard nje ya kikosi cha kwanza.

Caballero ni miongoni mwa wanasoka wanaopendwa na kustahiwa pakubwa na wenzake ugani Stamford Bridge. Anakuwa mchezaji wa pili baada ya fowadi matata mzawa wa Ufaransa, Olivier Giroud, 33, kutia saini mkataba mpya wa miezi 12 zaidi ugani Stamford Bridge, London Kaskazini.

Hadi kufikia sasa, mustakabali wa wachezaji Willian, 31, na Pedro Rodriguez, 32, kambini mwa Chelsea haujajulikana. Willian ambaye ni kiungo mzawa wa Brazil anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua Arsenal huku Pedro ambaye ni mzaliwa wa Uhispania, akihemewa na West Ham United na Leicester City. Mikataba ya wawili hao inatazamiwa kukatika rasmi ugani Stamford Bridge mnamo Juni 30, 2020.

Caballero alitarajiwa kuungana na wenzake uwanjani Conham, Uingereza kwa mazoezi ya kujiandaa kwa marejeo ya kivumbi cha EPL mnamo Juni 12. Kipa huyo ambaye pia amewahi kuchezea Malaga nchini Uhispania, alisajiliwa na Chelsea bila ada yoyote kutoka kambini mwa Manchester City mnamo 2017.