Michezo

CAF kutangaza wapinzani wa Gor na Kariobangi hapo Novemba 3

November 1st, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara 17 wa Ligi Kuu ya Kenya Gor Mahia na washindi wa Kombe la Ngao Kariobangi Sharks watafahamu wapinzani wao kwenye soka ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Mashirikisho hapo Novemba 3, 2018.

Gor ya kocha Dylan Kerr ilinyakua tiketi ya kushiriki Klabu Bingwa kwa mara ya pili mfululizo baada ya kushinda Ligi Kuu nayo Sharks ya kocha William Muluya ilichabanga Sofapaka 3-2 katika fainali ya SportPesa Shield.

Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) limetangaza Novemba 1 kwamba litafanya droo ya mashindano haya mawili jijini Rabat nchini Morocco katika mkutano wa kamati teule siku hiyo.

Gor, ambayo itaelekea nchini Uingereza mapema Novemba 2 kupepetana na Everton uwanjani Goodison Park hapo Novemba 6, ilishiriki Klabu Bingwa mwaka 2018. Ilichapa Leones Vegetarianos kutoka Equatorial Guinea katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 3-1.

Vijana wa Kerr walizimwa kwa jumla ya bao 1-0 dhidi ya Esperance ya Tunisia katika raundi ya kwanza. Iliteremka hadi Kombe la Mashirikisho ambapo ililemea SuperSport United kupitia bao la ugenini baada ya kuandikisha ushindi wa 1-0 jijini Nairobi na kulemewa 2-1 nchini Afrika Kusini.

Ilimenyana na Rayon Sports (Rwanda), Young Africans (Tanzania) na USM Alger (Algeria katika mechi za Kundi D. Gor ilifanya vizuri katika mechi zake nne za kwanza kabla ya kuteleza dhidi ya Rayon na USM Alger katika mechi mbili za mwisho na kubanduliwa nje. Hata hivyo, kwa kufika mechi za makundi za Kombe la Mashirikisho, Gor ilitunikiwa Sh27.9 milioni.