CAF yasukuma mbele fainali za AFCON 2023 kwa mwaka mmoja zaidi

CAF yasukuma mbele fainali za AFCON 2023 kwa mwaka mmoja zaidi

Na MASHIRIKA

MAKALA yajayo ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON) sasa yatafanyika nchini Ivory Coast mnamo 2024 badala ya mwaka ujao jinsi ilivyopangwa.

Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) chini ya rais Patrice Motsepe limeratibu upya kipute hicho kilichokuwa kitandazwe Juni-Julai 2023 kwa sababu ya huo utakuwa msimu wa mvua tele Ivory Coast.

“Hatuwezi tukahatarisha. Huku fainali za Kombe la Dunia zikifanyika nchini Qatar kati ya Novemba-Disemba mwaka huu, uamuzi wa kuahirisha kipute cha AFCON umechukuliwa badala ya kukileta mbele,” akasema Motsepe akiwa jijini Rabat, Morocco – mwenyeji wa Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWCON).

Ina maana kuwa fainali za AFCON zitanogeshwa kati ya Januari na Februari kwa mara ya pili mfululizo baada ya makala ya 33 mwaka huu kufanyika nchini Cameroon.

Mnamo 2017, CAF ilifichua mpango wa kuhamisha AFCON kutoka Januari-Februari hadi Juni-Julai ili kuepuka mizozo ya mara kwa mara na klabu za bara Ulaya zilizolazimika kuachilia masogora wa Afrika katikati ya msimu.

“Japo Januari si kipindi mwafaka kwa sababu ya klabu za Ulaya, ndilo chaguo la pekee tulilosalia nalo,” akaongeza Motsepe.

Chini ya rais Issa Hayatou aliyebanduliwa mamlakani mnamo 2017, CAF ilikataa kuidhinisha mapendekezo ya kubadilishwa kwa tarehe za kuandaliwa kwa AFCON.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CAF, Veron Mosengo-Omba, amesema hakuna mipango ya kudumu ya kurejesha fainali hizo hadi Januari-Februari kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya hali ya hewa barani kwa nyakati tofauti za mwaka.

Tangu rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, adokeze uwezekano wa kuanzishwa kwa mapambano ya African Super League, kipute hicho sasa kitanogeshwa Agosti 2023.

Mashindano hayo yatashirikisha timu 24 zitakazotuzwa jumla ya Sh11.7 bilioni huku mshindi akitia mfukoni Sh1.7 bilioni.

“Tuna idadi kubwa ya wawekezaji na wafadhili ambao wana azma ya kudhamini mashindano hayo,” akaongeza Motsepe.

CAF pia imesema michuano ya Klabu Bingwa Afrika, ambayo iko wazi kwa mataifa yote barani, itaendelea sambamba na kipute kipya cha ASL ambapo timu 24 bora zitapangwa kwa mujibu wa nafasi zao kwenye orodha ya viwango bora vya FIFA.

Baada ya kukosolewa pakubwa na wanafainali wa Klabu Bingwa Afrika, Al Ahly, kwa maamuzi ya kuandaa fainali ya 2021-22 katika uwanja wa nyumbani wa Wydad Casablanca waliotwaa ufalme, CAF pia imetangaza kuwa fainali ya mapambano hayo sasa yatarejea kuwa ya mikondo miwili.

Baada ya kipindi cha takriban nusu karne cha fainali ya Klabu Bingwa Afrika kuchezwa kwa mikondo miwili, mshindi wa kivumbi hicho alianza kuamuliwa kwa fainali ya mkondo mmoja pekee mnamo 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Joho ndiye chanzo cha shida zetu – Omar

TUSIJE TUKASAHAU: Wakulima wanaomba Nzoia Sugar iwalipe...

T L