Michezo

CAF yatoa tarehe mpya za vipute vya CHAN, AFCON

July 1st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Afrika (CAF) limethibitisha kwamba mechi za nusu-fainali na fainali ya kuwania ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika (Champions League) msimu huu sasa zitachezewa nchini Cameroon.

Isitoshe, shirikisho hilo limesisitiza kwamba fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zilizokuwa ziandaliwe nchini Cameroon mnamo Januari 2021 sasa zimeahirishwa hadi Januari 2022 na Cameroon watasalia kuwa wenyeji wa kipute hicho.

Maamuzi hayo yaliafikiwa katika kikao kilichoandaliwa mtandaoni mnamo Jumanne ya Juni 30, 2020 na kuhudhuriwa na maafisa wakuu wa CAF na wakuu wa mashirikisho yote wanachama wa CAF humu barani.

Kutokana na ugonjwa wa Covid-19, mabadiliko yafuatayo yamefanywa na CAF:

Fanali za AFCON 2021 sasa zimeahirishwa hadi Januari 2022 nchini Cameroon.

Fainali za CHAN 2020 ambazo hushirikisha wachezaji wanaosakata soka katika klabu zao za nyumbani pekee sasa zimeaahirishwa kutoka Septemba 2020 hadi Januari 2021.

Mechi za nusu-fainali na fainali za CAF Champions League ambazo kwa sasa zitakuwa za mkondo mmoja pekee msimu huu, zitasakatiwa nchini Cameroon. Mechi hizo zitashirikisha Al Ahly na Zamalek za Misri na Raja Casablanca na Wydad Casablanca za Morocco.

Mechi za nusu-fainali na fainali za CAF Confederations Cup ambazo kwa sasa zitakuwa za mkondo mmoja pekee msimu huu, zitachezewa nchini Morocco.

Mechi hizo zitashirikisha Pyramids FC (Misri), Horoya Conakry (Guinea), RS Berkane (Morocco) na Hassania Agadir (Morocco).