Michezo

Cape Verde watandika Msumbiji na kudhibiti kilele cha Kundi B katika Afcon

January 20th, 2024 1 min read

Na MASHIRIKA

TIAGO Manuel Bebe alifunga frikiki kutoka hatua ya 40 na kuongoza Cape Verde kutandika Msumbiji 3-0 katika mchuano wa pili wa Kundi B kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Ivory Coast.

Fowadi huyo wa klabu ya Rayo Vallecano nchini Uhiapania, aliwahi pia kuchezea Manchester United ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Nahodha Ryan Mendes alipachika wavuni bao la pili baada ya kuacha hoi kipa Ernan Siluane aliyezidiwa pia maarifa na Kevin Pina.

Ushindi wa Cape Verde uliwapa uhakika wa kumaliza kampeni za Kundi B kileleni mbele ya mabingwa wa zamani Misri na Ghana. Cape Verde almaarufu Blue Sharks watachuana na Misri katika mchuano wao wa mwisho mnamo Januari 22 wakifahamu kuwa watakutana na kikosi kitakachoambulia nafasi ya tatu kutoka Kundi A, C au D kwenye hatua ya 16-bora chini ya wiki moja ijayo.

Hata kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa fainali za Afcon nchini Ivory Coast kupulizwa, hakuna aliyefahamu kuwa Cape Verde wangeibuka washindi wa kundi lililojumuisha pia Misri na Ghana.

Kikosi hicho kinashikilia nafasi ya 73 kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa). Hii ni mara ya nne kwa Cape Verde kunogesha fainali za Afcon na wamesonga mbele kutoka hatua ya makundi katika makala matatu.

Cape Verde walipiga Ghana 2-1 katika mechi ya kwanza huku Msumbiji walio wa 111 duniani wakiambulia sare ya 2-2 dhidi ya Misri.

Bebe alianza kuchezea Cape Verde mnamo 2022 baada ya kubadilisha uraia wake kutoka Ureno. Misri na Ghana ambao wana alama mbili na moja mtawalia, huenda wote wakafuzu kwa raundi ya 16-bora kama vikosi vinne vilivyoridhisha zaidi makundini ila vikaambulia nafasi za tatu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO