Michezo

#CapeTown7s: Shujaa wamumunywa na Uingereza, Ufaransa na Fiji

December 8th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 inazidi kuwa mlima kwa Shujaa ya Kenya baada ya kupoteza dhidi ya Uingereza 29-12, Fiji 38-7 na Ufaransa 19-12 kwenye duru ya Cape Town Sevens katika Kundi C nchini Afrika Kusini, Jumamosi.

Vijana wa kocha Paul Murunga walivuta mkia katika duru ya ufunguzi mjini Dubai iliyoandaliwa Novemba 30 na Desemba 1 baada ya kupepetwa na Scotland (35-14), Ufaransa (21-17), Fiji (43-12), Uhispania (26-19) na Japan (26-19).

Mjini Cape Town, Kenya ilianza kwa kupepetwa 29-12 na Uingereza iliyovuna ushindi kupitia miguso ya Dan Norton (mitatu) na Ethan Waddleton na Phil Burgess. Tom Mitchell alichangia mikwaju miwili. Kenya ilifunga alama zake kupitia kwa Cyprian Kuto na Leonard Mugaisi na nahodha Eden Agero aliyepachika mkwaju.

Katika mechi ya pili dhidi ya Fiji, Kenya ilifungiwa katika nusu yake kwa kipindi kirefu na kuenda mapumzikoni ikiwa chini 24-0. Vincent Onyalla, ambaye aliitwa katika kikosi cha Cape Town kujaza nafasi ya Jeffery Oluoch aliyerejea Kenya baada ya duru ya Dubai Sevens, alifunga mguso wa kufutia machozi Fiji ikiongoza 38-0. Kenya ilinufaika kuona lango baada ya Fiji kusalia wachezaji sita uwanjani kufuatia kuadhibiwa kwa Meli Derenalagi kwa mchezo mbaya.

Kenya ilikamilisha siku ya kwanza kwa kulizwa na Ufaransa. Ilianza mchuano huu vyema kwa kuongoza 5-0 kupitia mguso wa Alvin Otieno dakika ya pili. Ufaransa ilienda mapumzikoni ikiongoza 12-5 baada ya kujibu kupitia miguso miwili kutoka kwa Thibaut Mazzoleni na Terry Bouhraoua na mkwaju wa Paulin Riva.

Kenya ilisawazisha 12-12 mapema katika kipindi cha pili kupitia mguso wa Otieno na mkwaju kutoka kwa Eden Agero. Hata hivyo, Riva alifunga mguso wa ushindi ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Jean Pascal Barraque zikisalia dakika mbili mechi kutamatika.

Fiji ilimaliza juu ya Kundi C baada ya kulipua Uingereza 21-19. Fiji na Uingereza ziliingia robo-fainali kuu kutoka kundi hili, huku Kenya na Ufaransa zikiteremka katika shindano la kupigania nafasi ya 9-16 (Challenge Trophy). Fiji ilibwaga Ufaransa 50-0 katika mechi yake ya ufunguzi. Duru ya Cape Town itakamilika Jumapili.