Habari Mseto

Capwell yawapa vipofu 75 wa Kiandutu chakula cha laki moja

June 9th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu itaendelea kuwajali watu wasiojiweza hasa vipofu na wazee.

Naibu Gavana Bi Joyce Ngugi amesema Jumanne kikundi hicho cha watu kimekuwa katika hali ngumu ya maisha na kwa sababu hiyo kampuni ya Capwell Ltd imejitolea kuwapa chakula vipofu katika kaunti hiyo.

Kampuni hiyo imewapa vipofu 75 wa kijiji cha Kiandutu chakula kilichogharimu Sh100,000.

“Tunashukuru sana wahisani ambao wengi wamejitolea kusaidia wakazi wa Kiambu kwa kuwapa chakula hasa wakati huu wa janga la Covid-19,” amesema Bi Ngugi.

Nao waendeshaji bodaboda wamekabidhiwa mavazi spesheli watakayovaa kutoa hamasisho jinsi janga la corona linavyoweza kuangamizwa.

“Tunajua wahudumu hao ni muhimu katika jamii na ni vyema kufanya kazi nao pamoja. Hata wamepewa sanitaiza ili waweze kudumisha usafi wakati wowote wanapowabeba wateja wao,” amesema Bi Ngugi.

Amesema Kaunti ya Kiambu inalenga kuzuru vijiji vilivyoathirika kiuchumi kama Kiandutu, Gatuanyaga na Matharau.

Amesema licha ya kaunti kusambaza chakula kwa walioathirika pia serikali hiyo inaendelea kuwahamasisha jinsi ya kudumisha usafi kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

Diwani wa mji wa Thika Bw Andrew Kimani amepongeza juhudi za kaunti ya Kiambu kuona ya kwamba inawajali walioathiriwa.

Ametoa wito kwa walioathirika kama wazee, walemavu na vipofu wakae nyumbani badala ya kujumuika na watu wengi mjini.

“Ninatoa wito kwa jamaa za makundi yaliyo katika hatari kubwa kuhakikisha wanasalia kuwa salama,” amesema Bw Kimani.