CARABAO: Arsenal, Chelsea kulimana na Liverpool na Manchester United

CARABAO: Arsenal, Chelsea kulimana na Liverpool na Manchester United

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KLABU za Arsenal na Chelsea zinakabiliwa na mtihani mgumu kusonga mbele kwenye mashindano ya League Cup baada ya kukutanishwa dhidi ya Liverpool na Manchester United, mtawalia.

Katika droo ya raundi ya 16-bora iliyofanywa baada ya mechi za raundi ya tatu kutamatika Jumatano, Arsenal ya kocha Unai Emery itapimwa vilivyo na vijana wa Jurgen Klopp uwezo wake wa kushindania taji itakapoalikwa uwanjani Anfield mnamo Oktoba 29.

Viongozi wa Ligi Kuu Liverpool, ambao wanashikilia rekodi ya mataji mengi ya League Cup (manane), walizaba Milton Keynes Dons 2-0 Jumatano kupitia mabao ya James Milner na Ki-Jana Hoever na kuingia raundi hii ya nne.

Arsenal, ambayo ni nambari nne ligini, ilipepeta Nottingham Forest 5-0 Jumanne kupitia mabao ya Gabriel Martinelli (mawili), Rob Holding, Joe Willock na Reiss Nelson.

Vijana wa Emery tayari wameonjeshwa makali ya Liverpool msimu huu waliponyamazishwa 3-1 ligini mnamo Agosti 24. Mabingwa hawa wa League Cup mwaka 1987 na 1993 hawana ushindi dhidi ya Liverpool katika mechi tisa zilizopita.

Wafalme mara tano United, ambao walishinda mashindano haya ya muondoano mara ya mwisho mwaka 2017, walisonga mbele kupitia mikwaju ya penalti 5-3 dhidi ya klabu ya daraja ya tatu Rochdale baada ya muda wa kawaida kumalizika 1-1 uwanjani Old Trafford.

Mambo yalikuwa nywee kwa washindi mara tano Chelsea, ambao waliaibisha Grimsby 7-1 kupitia mabao ya Michy Batshuayi (mawili), Ross Barkley, Pedro, Kurt Zouma, Reece James na Callum Hudson-Odoi. Matt Green alifunga bao la Grimsby kufutia machozi.

United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer ilianza msimu mpya kwa kupepeta Chelsea 4-0 mnamo Agosti 11. Timu ya United na Chelsea zinashikilia nafasi za nane na 11 ligini mtawalia kwa alama nane kila mmoja. United haijapoteza dhidi ya Chelsea katika mechi nne zilizopita.

Kibarua kigumu

Zawadi ya Southampton kushindia majirani na mahasimu wao wakuu Portsmouth ugenini kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 35 ni kupepetana dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City.

Vijana wa Pep Guardiola wamelemea Southampton katika mechi tano zilizopita kwa hivyo Southampton watakuwa na kibarua kigumu.

Klabu zingine kutoka Ligi Kuu zilizokutanishwa katika League Cup ni Everton dhidi ya Watford nayo Aston Villa italimana na Wolves.

Mechi hizi zinaweza kuenda upande wowote.

Msimu uliopita, Everton ilichapwa na Watford ugenini 1-0 na kulipiza kisasi kwa dozi sawa na hiyo ilipokuwa nyumbani Goodison Park.

Timu mbili zisizo za Ligi Kuu zilizosalia mashindanoni, Crawley na Colchester, zilibahatika kukutanishwa. Zinashiriki ligi ya daraja ya nne. Nayo Leicester itazuru Burton, huku timu za Ligi ya Daraja ya tatu Oxford na Sunderland zikilimana katika mchuano mwingine wa kuingia robo-fainali.

You can share this post!

NI MTIMKO! Riadha za Dunia kutifua vumbi Doha

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Dhana mbaya ina uwezo wa kuua udugu...

adminleo