CARABAO CUP: Arsenal walazimishia Liverpool sare tasa katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali

CARABAO CUP: Arsenal walazimishia Liverpool sare tasa katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta alikuwa mwingi wa sifa kwa vijana wake wa Arsenal baada ya kujituma maradufu na kuwalazimishia Liverpool sare tasa katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali za Carabao Cup ugani Anfield mnamo Alhamisi usiku.

Arsenal walitandaza mchuano huo kwa zaidi ya dakika 70 wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya kiungo mkabaji Granit Xhaka kuonyeshwa kadi nyekundu kwa hatua ya kumchezea visivyo Diogo Jota alipojaribu kuzuia krosi ya Andrew Robertson kumfikia fowadi huyo raia wa Ureno.

Tukio hilo nje ya kijisanduku liliwapa Liverpool frikiki iliyopaishwa na beki Trent Alexander-Arnold. Licha ya wachezaji wa Arsenal kupunguzwa na kikosi kujipata katika presha ya kudhibiti Liverpool, vijana wa Arteta ndio walikuwa wa kwanza kuelekeza kombora lililonga shabaha langoni mwa wenyeji wao.

Ushirikiano mkubwa kati ya Bukayo Saka na Alexandre Lacazette ulitatiza safu ya nyuma ya Liverpool waliopoteza nafasi nyingi za wazi kupitia Takumi Minamino na Jota waliojaza nafasi za Mohamed Salah na Sadio Mane wanaowajibikia Misri na Senegal mtawalia kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zinazoendelea nchini Cameroon.

Mechi ya mkondo wa pili kati ya Arsenal na Liverpool sasa itasakatiwa ugani Emirates mnamo Alhamisi ya Januari 20, 2022. Mshindi atakutana na Chelsea ya kocha Thomas Tuchel kwenye fainali itakayofanyika ugani Wembley mwishoni mwa Februari 2022. Chelsea walijikatia tiketi ya fainali baada ya kudengua Tottenham Hotspur kwa jumla ya mabao 3-0 kwenye hatua ya nusu-fainali.

Mchuano wa mkondo wa kwanza uliokuwa ukutanishe Liverpool na Arsenal uliahirishwa hadi Januari 20, 2022 baada ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona kushuhudiwa kambini mwa Liverpool.

Huku Liverpool walikosa maarifa ya Salah na Mane, Arsenal walikuwa bila huduma za viungo Martin Odegaard anayeugua Covid-19 pamoja na Thomas Partey ambaye sasa anachezea Ghana katika fainali za AFCON nchini Cameroon.

Wawili hao, pamoja na Xhaka, sasa watakosa gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litakalokutanisha Arsenal na Tottenham Hotspur ugenini mnamo Januari 16, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kipaji cha beki huyu chaimarika kadri anavyojituma

AFCON: Cameroon watandika Ethiopia na kufuzu kwa hatua ya...

T L