Makala

Caroline Murigu: Ustahimilivu umemfanikisha katika ufugaji wa kuku

February 20th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KWA muda wa miaka miwili ambayo imepita kilimo cha ufugaji wa kuku nchini kimekuwa kikipitia changamoto zisizomithilika.

Soko la mazao yake ambayo ni mayai na nyama, limedorora kwa kiasi kikubwa kwa kile kinachotajwa kama kufurika kwa mayai na kuku wa nyama kutoka nje ya Kenya.

Mwaka 2018 baadhi ya wafugaji wa ndege hawa pamoja na wadau husika waliandaa warsha kadhaa ili kutathmini jinsi ya kuangazia suala hili.

Kuna wafugaji ambao wameshurutika kuacha shughuli hii baada ya kukadiria hasara chungu nzima. Hata hivyo, kero hili halijazima ndoto za Caroline Murigu ambaye ni mfugaji wa kuku wa mayai wa kisasa almaarufu Hybrid Layers.

Unapozuru mradi wake ulioko eneo la Kamakis, By-Pass Ruiru kaunti ya Kiambu, utakaribishwa na sauti za kuku zinazohinikiza anga ya mazingira yake. Mapenzi yake kwa kuku na kwa madhumuni ya kuondoa upweke katika boma lake ndiyo yalimchochea kuwafuga.

“Ninapenda kuku kwa dhati, huchangamsha boma langu kwa kelele,” aeleza Bi Murigu.

Kizimba chake chenye ukubwa wa mita 40-urefu na mita 35-upana kimesitiri kuku wapatao 600.

Mtaji

Alianza ufugaji mwaka wa 2018 kwa kuku 500 aliouziwa Sh150 kila mmoja wakiwa vifaranga pamoja na gharama ya kuunda kizimba, vifaa vya lishe na maji, na matibabu kwa jumla ikifikia Sh350,000.

Aidha, walikuwa kuku wa kienyeji wa kisasa wa kutaga mayai na wa nyama.

“Miezi minne baadaye 100 walifariki, waliosalia nikawauza Sh700 kila mmoja. Utangulizi haukuwa rahisi kamwe kwa kuwa nilipokokotoa hesabu kuku mmoja alitumia wastani wa Sh400 kwa chakula,” afafanua.

Kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa mapishi, licha ya pigo hilo Bi Murigu hakufa moyo.

“Awamu ya pili niliweka wa nyama pekee niliowauza wiki sita baadaye,” aeleza.

Bi Caroline Murigu, mfugaji wa kuku wa kisasa wa mayai, Ruiru, Kiambu. Picha / Sammy Waweru

Kuku alionao kwa sasa (600) ni wa mayai, wanaotaga kwa muda wa miaka miwili mfululizo kisha wanageuzwa kuwa wa nyama. Kundi hili, aliwanunua wakiwa jumla ya 800 lakini kufikia sasa 200 wamefariki.

Jeremiah Njuguna, mtaalamu wa masuala ya biashara na uchumi anasema katika uwekezaji wowote ule unahitaji uvumulivu ili kuafikia malengo. Kuhusu pandashuka alizopitia Bi Murigu alipoanza safari ya kilimo cha kuku, mtaalamu huyu anasema ni jambo la kawaida katika utangulizi wa biashara na kwamba kabla ya kung’oa nanga haja ipo kufanya utafiti wa kutosha ili kujua changamoto ibuka.

“Kilimo ni mojawapo ya sekta ya kuwekeza, unapaswa kutembelea waliofanikisha jitihada zao. Pia kuna utafiti kupitia mitandao na kuhudhuria warsha,” ashauri Bw Njuguna.

Bima

Pili, mwekezaji akifahamu wazi biashara haikosi hasara mbali na faida, anahimizwa kuisajili katika mashirika ya bima.

“Waliosajili biashara zao mikasa inapotokea huwa rahisi kufidiwa,” asema.

Wakati wa mahojiano mfugaji Bi Murigu alisema kupitia hadithi za wafugaji tajika kama Caleb Karuga, za milima na mabonde waliyopitia humpa motisha kutokata tamaa.

Ili kufanikisha ufugaji wa kuku, wataalamu wa masuala ya kilimo na ufugaji wanasisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi wa mazingira ya makazi yake, lishe bora na maji.

“Matibabu ni kigezo muhimu kutilia maanani kwa mifugo. Kudhibiti magonjwa na vimelea, usafi uwe wa hadhi ya juu, na wanapougua tafuta ushauri kutoka kwa mtaalamu,” ahimiza Veronicah Kirogo, mtaalamu wa kilimo.

Anaongeza kusema kuwa kizimba cha kuku kiwe na nafasi ya kutosha ili kuepuka msongamano. Kuku mmoja anapaswa kuwa na nafasi ya futi 2 kwa 2 mraba.