Makala

CAROLYNE KIARIE: Raha yangu ni kumfikia Gabriel Union katika uigizaji

July 17th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ALITAMANI kuhitimu kuwa mwalimu hasa kufunza somo la Kiingereza, ambapo hadi sasa anadhamiria kusomea taaluma ya ualimu miaka ijayo.

Hata hivyo anajivunia kutunikiwa talanta ya maigizo ambayo imeibuka tegemeo lake tangu alipotamatisha elimu ya sekondari katika shule ya Komothai Girls, Kaunti ya Kiambu.

Carolyne Wairimu Kiarie ni binti mwenye tabasamu ya kuvutia ambaye katika masuala ya maigizo analenga kumfikia mwandishi wa vitabu, mwanaharakati na mwigizaji shupavu mzawa wa Marekani, Gabriel Union.

Anasema huvutiwa na uhusika wake staa huyo ambaye ameshiriki filamu nyingi tu ikiwamo ‘She’s All That,’ ‘Abandon,’ ‘The Brothers,’ ‘Deliver Us From Eva,’ na ‘Two Can Play That Game,’ kati ya zingine.

”Nilianza kujituma kwenye masuala ya maigizo nikiwa mwanafunzi maana nakumbuka mwaka 2007 niliibuka mwigizaji bora shuleni,” anasema na kuongeza kwamba kipindi hicho alitunga mchezo wa kuigiza uliofanikiwa kutinga fainali za mkoa wa kati kwenye mashindano ya shule za sekondari.

Kisura huyu ambaye kwa sasa amezamia uigizaji wa sauti kwenye stesheni za redio hapa nchini aliwahi kufanya kazi na brandi tofauti ikiwamo ELJAY Production walikozalisha filamu kwa jina Kelele FM iliyopeperusha kupitia runinga ya K24.

Pia anajivunia kushiriki filamu ‘Gereji matata’ na kuonyeshwa kupitia runinga ya K24 na MaishaMagic East. Kadhalika chini ya Kikwetu Productions alishiriki filamu kama Maisha bure-Maisha Magic East, Maisha bure-QTV, Senior Pastor – Maisha Magic East, Housemates -K24 na Maisha Magic East bila kuweka katika kaburi la sahau Tax Driver -Maisha Magic East kati ya zingine.

Mwigizaji Carolyne Wairimu Kiarie. Picha/ John Kimwere

Binti huyu aliwahi kuteuliwa kuwania tuzo mbali mbali katika uigizaji kupitia filamu alizowahi kushiriki zikiwamo ‘Senior Pastor,’ ‘Maisha bure,’ na ‘Housemates.’

Katika mpango mzima anasema analenga kumiliki brandi ya kuzalisha filamu ili kukuza wenye vipaji vya waigizaji wanaokuja wavulana na wasichana.

Kisura huyu siyo mchoyo wa mawaidha. Anashauri waigizaji wanaoibukia kuwa nyakati zote wanapopata nafasi kushiriki filamu yoyote wawe wakionyesha ujuzi wao kwa kujitolea maana hawafahamu watakaopata mwanya kuzitazama.

”Waigizaji wale wageni kwenye gemu kamwe hawapaswi kudharau brandi inayowapa nafasi kuonyesha talaamu zao maana huenda itasaidia kufungua milango ya mafanikio,” alisema na kuongeza kuwa hawapaswi kuwa wepesi wa kutaka tamaa.

Je, binti huyu amekubana na changamoto gani? Mwigizaji huyu anasema mwanzoni wengi wao hupitia wakati mgumu hasa baada ya malipo yao kucheleweshwa ambapo wakati mwingine hujipata njiapanda mbele ya jamaa za familia zao.

”Kusema kweli tunaposhindwa kugharamia mahitaji ya kimsingi hugeukia jamaa za familia zetu kuomba msaada lakini baadhi yao huanza kutotuamini na kupendekeza kuacha maigizo,” alisema na kuongeza kwamba hali hiyo huwavunja moyo waigizaji chipukizi.