Michael Carrick aondoka Man-United baada ya kusimamia klabu hiyo katika mechi tatu bila kupoteza

Michael Carrick aondoka Man-United baada ya kusimamia klabu hiyo katika mechi tatu bila kupoteza

Na MASHIRIKA

MICHAEL Carrick ameondoka kambini mwa Manchester United baada ya kipindi chake cha kuwa kocha wa muda wa kikosi hicho kukamilika.

Carrick amesimamia michuano mitatu ya Man-United tangu kocha Ole Gunnar Solskjaer atimuliwe.

Aliongoza miamba hao kupepeta Villarreal ya Uhispania 2-0 kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla ya kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Chelsea na ushindi wa 3-2 dhidi ya Arsenal kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kuondoka kwa Carrick kunajiri baada ya Man-United kuajiri kocha Ralf Rangnick kushikilia mikoba yao hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22.

“Baada ya kushauriana na wadau wengine na kufikiria kwa kina kuhusu jambo hili, nimeamua kwamba sasa ndio wakati mwafaka zaidi wa kuagana na Man-United,” akasema sogora huyo wa zamani.

Akichezea Man-United kwa miaka 12, Carrick alisaidia kikosi hicho kutwaa mataji matano ya EPL na moja la UEFA mnamo 2008. Anabanduka ugani Old Trafford baada ya ushindi dhidi ya Arsenal kukweza Man-United hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Corona yafagia asilimia 35 ya biashara ndogo

Wataka suti tu!

T L