Michezo

Casillas amkejeli Mourinho baada ya kudhalilishwa Anfield

December 17th, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

UBISHI kati ya mnyakaji wa FC Porto Iker Casillas na kocha wa Manchester United Jose Mourinho unazidi kutokota baada ya ‘nyani’ huyo kumdhihaki mkufunzi wake wa zamani kutokana na  kichapo cha 3-1 mikononi mwa LiverPool Jumapili Disemba 16 ugani Anfield.

Casillas hakuwahi kupatana wala kuelewana na Mourinho wakati akiwa kipa wa Real Madrid baada ya kocha huyo kumlisha benchi bila sababu na kutumia sana huduma za kipa chaguo la pili wa Madrid wakati huo Diego Lopez.

Majuma matatu yaliyopita, Mourinho alishtumu mahojiano kati ya Casillas na mwanahabari Jorge Valdona akisema ‘’Haya ni mahojiano ya mtu ambaye taaluma yake ya soka inaelekea ukingoni,”

Hata hivyo kipa huyo alimjibu Mourinho kwa madharau baada ya kufungwa na Liverpool siku ya Jumapili akisema “Kwa kuangazia makocha, ni  wapi na lini mnatambua kwamba hawahusiki tena katika kusimamia timu au mazoezi ya timu?”.

Kichapo alicholishwa Mourinho na Manchester United yake sasa kinamzidishia presha ya kubwaga manyanga huku ikisemekana wachezaji wengi wanamchukia na hawapendezwi na mbinu zake za ukufunzi.