Kimataifa

Catherine, mke wa mwanamfalme William augua saratani

March 22nd, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MKE wa mwanamfalme William, Catherine wa Wales, amesema kuwa yuko kwenye hatua za mwanzo za matibabu, baada ya uchunguzi wa kimatibabu kubaini kwamba anaugua saratani.

Kwenye ujumbe aliotoa kwa njia ya video mnamo Ijumaa, Catherine ambaye pia anajulikana kwa jina Kate Middleton, alisema hali hiyo “ilikuwa mshangao sana kwake”  baada  ya “miezi kadhaa ya mahangaiko makubwa.”

Hata hivyo, alisema “ana nguvu na anaendelea kupata nafuu kila siku.”

Maelezo zaidi kuhusu saratani hiyo hayakutolewa, ijapokuwa Makao ya Kifalme ya Kensington yalisema yanaamini kuwa atapata nafuu.

Taarifa hiyo ilisema kuwa wakati mwanamfalme huyo alifanyiwa upasuaji wa tumbo mnamo Januari, haikujulikana angepatikana na saratani.

“Hata hivyo, chunguzi kadhaa baada ya upasuaji, ilibainika nina saratani. Madaktari wangu walinishauri kwamba ninafaa kufanyiwa tiba ya kemikali (kemotherapi). Kwa sasa, niko katika hatua za mwanzo za matibabu hayo,” akasema.

Matibabu hayo yalinza mwishoni mwa mwezi Februari. Makao ya kifalme yalisema kuwa hayatatoa maelezo zaidi ya kibinafsi ya matibabu yake, ikiwemo aina ya saratani anayougua mwanamfalme  huyo.

Catherine, 42, alisema amekuwa akifikiria kuhusu wale wote ambao wameathiriwa na saratani, akiongeza: “Kwa wale wanaokabiliwa na mardhi haya, tafadhali msife moyo au matumaini. Hamko peke yenu.”

Hilo linajiri mwezi mmoja baada ya Kasri la Buckingam kusema mnamo Februari kwamba Mfalme Charles III alithibitishwa kuugua saratani ya kibofu.

William ndiye yuko mstari wa mbele kurithi ufalme wa Uingereza kutoka kwa babake, Charles.