Makala

CATHERINE NYOKABI: Ndoa ya harusi ilivyoishia kwa talaka

February 15th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

VISA vya unyanyasaji na dhuluma za kijinsia nchini katika miaka ya hivi punde vimeonekana kuongezeka.

Nyingi ya visa hivi vinashuhudiwa katika ndoa na uhusiano wa kimapenzi. Baadhi ya wahusika wameripotiwa kupotea, miili yao kupatikana imetupwa baada ya kuuawa kikatili na kwa njia isiyoeleweka.

Akivuta mawazo yake nyuma, Catherine Nyokabi anasema kwa wakati mmoja alikuwa katika ndoa iliyojawa na uchungu wa moyo. Mapenzi yake yalikuwa afunge ndoa na kuanzisha familia atakayoonea fahari akihusishwa nayo, lakini hayo hayakutimia.

“Tulifanya harusi 2007 nikiwa na umri wa miaka 26, nilitamani kuwa na familia sawa na nilivyoona wazazi wangu wakiishi kwa upendo na amani,” asema Nyokabi, anayependa kujitambua kama Cate. Miezi na miaka ya kwanza katika ndoa huwa yenye furaha, na anasimulia kwamba alikuwa na kila sababu ya kutabasamu.

Ndoa inapoingia doa wahusika; mume na mke, ndio hufahamu fika kiini chake. Ingawa kuna vijisababu kama ukosefu wa uaminifu miongoni mwao, unyanyapaa-presha ya utengano kutoka kwa wazazi, mashemeji, marafiki na hata wafanyakazi wenza ikiwa hawaridhiki.

Catherine Nyokabi alipohojiwa na Taifa Leo Dijitali. Picha/ Sammy Waweru

Vilevile, pandashuka katika familia hujiri iwapo kuna asiyetekeleza majukumu yake kikamilifu hivyo basi kusababisha mvutano.

Miaka kadhaa baada ya Cate na mume wake kufunga nikahi, ndoa yao ilianza kuingia doa. Weledi wa semi walilonga ‘kikulacho ki nguo nguoni mwako’, kulingana na mwanadada huyu ambaye ni mama wa mtoto mmoja ni kwamba aliyeteka mume wake kimawazo ni mmoja wa wasichana walioisimamia harusi yao.

Hakuna kinachouma na kukereketa maini kama kuona mchumba ameelekeza mapenzi yake kwingine, na Cate anaeleza kuwa hili ni suala lililohangaisha moyo wake. Wengi wanapojipata katika hali hii hufikiria kulipiza kisasi, aidha kwa kutafuta mpango wa pembeni, kutendea mwenzake unyama au aliyemnasa mwenzake kwa sababu ya ghadhabu.

Licha ya Cate kujaribu kadri awezavyo kunusuru ndoa yake kwa kuhusisha wataalamu wa masuala ya familia, pasta na wazazi kutoka pande zote mbili, mambo yaligonga mwamba. Anafichua kuwa mwaka wa 2013, yeye na mume wake waliafikiana kutalakiana, uamuzi ambao ulikuwa mithili ya kutafuna tembe kali.

“Mimi ni mcha Mungu, na kulipiza kisasi si suluhu. Hata Biblia inaruhusu ndoa ikikosa uaminifu, talaka inaruhusiwa, sikuwa na budi ila kuchukua mkondo huo. Kwa kufanya hivyo, mauaji tunayosikia kila uchao hayatashuhudiwa,” anaeleza. Picha/ Sammy Waweru

Elizabeth Mwangi, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ndoa na kifamilia anasema kinachosambaratisha familia nyingi ni ukosefu wa mawasiliano. Shida zinapoanza kuibuka, haja ipo wahusika kuwasiliana kwa njia ifaayo na kwa mujibu wa Bi Mwangi ni hatua za kwanza muhimu kunusuru ndoa.

“Kimya ni kama kiambaza, hutaweza kujua kinachofanyika nyuma yake, mawasiliano ndiyo njia ya kutatua migogoro,” aeleza mdau huyu, akihimiza mambo yanapokuwa magumu wataalamu wa kifamilia wahusishwe.

“Ndoa inapoingia unyanyapaa na vita vya mara kwa mara, wahusika wanashauriwa kuachana ili kuepuka maafa,” aongeza Bi Mwangi.

Cate anasema hatua waliyochukua ilimfungua kutoka kwa minyororo inayotunga usaha, wanandoa wafikiriapo kutendeana unyama.

Baada ya kutalakiana, utangulizi haukuwa rahisi ikizingatiwa kwamba alikuwa na mtoto aliyemtegemea. “Mungu alinifungulia milango ya heri, mtoto wangu hakulala njaa,” aelezea.

Hadithi yake inawiana na ya Lucy Wambui Gathungu, ambaye alilazimika kugura ndoa akilalamika kwamba yake ilisheheni dhuluma na vita vya kijinsia. “Nilijaaliwa watoto wawili na siku nyingi tulilala bila chakula kwa sababu bwana hakuwajibikia majukumu,” asema Wambui.

Catherine Nyokabi katika shamba lake la kabichi. Picha/ Sammy Waweru

Anaongeza, “Nilianza kwa vibarua vya dobi na kulimia watu mashamba. Niliweka akiba na hatimaye nikawa mkulima.” Bi Wambui ni mkulima tajika wa mboga kaunti ya Nyeri.

Kwa upande wake Cate anasema hajafa moyo kurejea katika ndoa, japo na mume anayemheshimu. “Ninaamini ndoa ikipata wachumba walio tayari kuanzisha familia, waelewane na kupendana itafanikiwa,” aeleza mjasirimali huyu.

Bali na kuwa mkulima wa matunda aina ya matofaha Nyeri, anafanya biashara jijini Nairobi ikiwa ni pamoja na kuuza miche ya matofaha nje ya Kenya. Barani Afrika, amezuru mataifa kama Botswana, Uganda, Misri, Tanzania na Nigeria kwa madhumuni ya kutoa mafunzo ya kilimo cha matofaha.

Anahimiza wanawake wenza hasa walio kwenye ndoa kusaidia waume wao kutekeleza majukumu. “Kuna njia nyingi za kuweka akiba kama vile vyama vya ushirika na makundi, kina mama wajiunge navyo ili waweze kuimarisha familia zao,” ashauri.

Dhuluma za kimapenzi haziathiri wanawake pekee, pia kuna wanaume wanaopitia unyanyapaa. Wanashauriwa kutafuta mawaidha kutoka kwa wataalamu wa masuala ya ndoa.