Michezo

Cavani aahidi kufufua makali ya Manchester United

October 6th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wamemsajili fowadi wa zamani wa Paris Saint-Germain (PSG), Edinson Cavani, 33, bila ada yoyote.

Nyota huyo raia wa Uruguay aliyeondoka PSG mwishoni mwa Juni alitia saini mkataba wa mwaka mmoja kambini mwa Man-United mnamo Oktoba 5, 2020.

Kutua kwake ugani Old Trafford kunatazamiwa kuimarisha safu ya mbele ya Man-United ambao imekuwa ikiongozwa na washambuliaji chipukizi Marcus Rashford, Anthony Martial na Mason Greenwood.

Hadi kuingia kwake Man-United, Cavani alikuwa amefunga jumla ya mabao 341 kutokana na mechi 556 alizocheza katika kiwango cha klabu. Mabao 200 kati ya hayo yalitokana na mechi 301 alizopigia PSG ambao ni miamba wa soka ya Ufaransa. Cavani anajivunia pia kufungia timu ya taifa ya Uruguay jumla ya mabao 50 kutokana na mechi 116.

Huenda kibarua chake cha kwanza kambini mwa Man-United ni gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) litakalowakutanisha na PSG mnamo Oktoba 20, 2020 uwanjani Parc de Princes, Ufaransa. Man-United wametiwa katika zizi moja na PSG, RB Leipzig na Istanbul Basaksehir kwenye hatua ya makundi ya kipute cha UEFA msimu huu.

Kabla ya hapo Man-United watakuwa wamekutana na Newcastle United kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 17, 2020. Mchuano huo utakuwa wa kwanza baada ya pumziko fupi litakalokuwa limepisha mechi za kimataifa.

Kufikia sasa, Man-United inayotiwa makali na kocha Ole Gunnar Solskjaer inashikilia nafasi ya 16 kwenye msimamo wa jedwali la EPL baada ya kujizolea alama tatu pekee kutokana na michuano mitatu ya ufunguzi wa kampeni za muhula huu.

Man-United walipokezwa kichapo cha 6-1 katika mechi yao ya mwisho ya EPL dhidi ya Tottenham Hotspur mnamo Oktoba 4, 2020 uwanjani Old Trafford.

“Man-United ni mojawapo ya klabu kubwa zaidi duniani. Ni tija na fahari tele kuwa sehemu ya kikosi hiki,” akasema Cavani huku akiwa mwingi wa matumaini kwamba atatamba zaidi ndani ya jezi za waajiri wake wapya.

Ingawa PSG walikuwa radhi kurefusha kipindi cha kuhudumu kwake ugani Parc des Princes, kuondoka kwake kambini mwa wanafainali hao wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019-20 kulichochewa na mizozo ya mara kwa mara kati yake na mshambuliaji Neymar Jr.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, mshahara ambao Cavani atakuwa akilipwa ugani Old Trafford hautavuruga mfumo wa sasa jinsi ambavyo ujio wa Alexis Sanchez ulifanya baada ya kuagana na Arsenal mnamo Januari 2018.

Hadi alipojiunga na Inter Milan, Sanchez ambaye ni raia wa Chile, alikuwa akilipwa ujira wa hadi Sh49 milioni kwa wiki uwanjani Old Trafford.

Licha ya ukubwa wa umri wa Cavani, kocha Ole Gunnar ameshikilia kwamba sogora huyo ataleta tajriba pevu na uzoefu utakaochangia pakubwa makuzi ya wanasoka chipukizi kambini mwa Man-United.

Japo kusajiliwa kwa Cavani kutafanya Man-United kukashifiwa pakubwa na wakosoaji wao, Solskjaer ameshikilia kuwa rekodi nzuri ya sogora huyo mbele ya malango ya wapinzani ni kiini cha usimamizi kumhemea.

Kusajiliwa kwa Cavani kutarejesha kumbukumbu za 2016 ambapo Man-United walimsajili fowadi mkongwe Zlatan Ibrahimovic akiwa na umri wa miaka 34. Ibrahimovic kwa sasa anachezea AC Milan ya Italia akiwa na umri wa miaka 39. Nyota huyo raia wa Uswidi hakuridhisha kambini mwa Man-United baada ya kupachika wavuni mabao 29 kutokana na mechi 53 alizozisakata kati ya 2016 na 2018.