Michezo

Cavani atokea benchi kuiongeza Man-United nguvu za kupiga Southampton

November 30th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

EDINSON Cavani alitokea benchi na kuchochea Manchester United kutoka nyuma kwa mabao mawili na kupepeta Southampton 3-2 uwanjani St Mary’s mnamo Novemba 29, 2020.

Cavani, 33, alitokea benchi katika kipindi cha pili kujaza nafasi ya chipukizi Mason Greenwood. Ushawishi wa fowadi huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain (PSG) ulihisika pakubwa katika kipindi kifupi cha ujio wake uwanjani na akafunga mabao mawili yaliyofuta juhudi za awali za Southampton waliokuwa wamefungiwa na Jan Bednarek na James Ward-Prowse.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer aliyewalaumu wachezaji wake kwa kupoteza nafasi nyingi za wazi katika mchuano huo, alilazimika pia kumwondoa kipa David De Gea mwishoni mwa kipindi cha kwanza na nafasi yake kutwaliwa na chipukizi Dean Henderson.

Cavani alishirikiana vilivyo na kiungo Bruno Fernandes aliyewafungia Man-United bao la kwanza dhidi ya Southampton katika dakika ya 60.

Ushindi kwa Man-United uliwapaisha hadi nafasi ya nane kwa alama 16 sawa na Everton ya kocha Carlo Ancelotti. Kwa upande wao, Southampton kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano kwa pointi 17 sawa na Wolves waliowang’ata Arsenal 2-1 ugani Emirates.

Southampton kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Brighton mnamo Disemba 7 huku Man-United wakitarajiwa kuwa wenyeji wa PSG kwenye gozi la UEFA mnamo Disemba 2 kabla ya kuwaendea West Ham United mnamo Disemba 5, 2020.

Hadi kuingia kwake Man-United mnamo Oktoba 2020, Cavani alikuwa amefunga jumla ya mabao 341 kutokana na mechi 556 alizocheza katika kiwango cha klabu. Mabao 200 kati ya hayo yalitokana na mechi 301 alizopigia PSG ambao ni miamba wa soka ya Ufaransa. Cavani anajivunia pia kufungia timu ya taifa ya Uruguay jumla ya mabao 50 kutokana na mechi 116.

“Man-United ni mojawapo ya klabu kubwa zaidi duniani. Ni tija na fahari tele kuwa sehemu ya kikosi hiki,” akasema Cavani huku akiwa mwingi wa matumaini kwamba atatamba zaidi ndani ya jezi za waajiri wake wapya baada ya kufungua rasmi akaunti yake ya mabao.