Michezo

CAVANI TAMAA YA CHELSEA: Kocha Frank Lampard amtaja Edinson 'mchezaji aliyekamilika'

January 22nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Frank Lampard amemtaja Edinson Cavani kama mwanasoka aliyekamilika, siku chache tu baada ya habari kuchipuza kuwa mkufunzi huyo wa Chelsea anatamani klabu imsajili raia huyo wa Uruguay.

Chelsea ilikubaliwa kusajili wachezaji wapya mwezi huu, baada ya marufuku ya miaka miwili waliyopewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kupunguzwa kwa miezi 12 na Mahakama ya Kusikiza Malalamishi ya Michezo.

Cavani ambaye ana umri wa miaka 32 atakuwa mchezaji huru kufikia mwisho wa msimu huu, na tayari ameomba klabu yake ya Paris Saint-Germain nchini Ufaransa imkubalie kuondoka.

Ombi lake limechangiwa na timu kadhaa kuonyesha dalili za kumtaka, ikiwemo Atletico Madrid ya La Liga nchini Uhispania.

“Niliwahi kucheza dhidi yake na daima nafurahia mwelekeo na mtazamo wake, mbali na rekodi yake nzuri ya ufungaji mabao. Kwa sasa siwezi kusema zaidi kuhusu hali yake, lakini hebu tusubiri tuone kitakachotokea,” alisema Lampard.

“Wazo la kusajili mastaa walio na ujuzi wa kutosha ni miongoni mwa mipango yangu kwa sasa, kwa sababu wachezaji chipukizi kama wale nilionao katika timu wanahitaji watu wa kuwasaidia uwanjani. Iwapo mpango kama huo utatusaidia, basi tutafanya hivyo,” aliongeza.

Mbali na Chelsea, Manchester United pia wamehusishwa na Cavani, ambaye kufikia sasa amefunga jumla ya mabao 351 katika mechi 577, pamoja na mengine 50 aliyofungia timu yake ya taifa ya Uruguay katika mechi 116.

Tangu ajiunge na PSG akitokea Napoli kwa mkataba wa Sh6.6 bilioni mnamo 2013, nyota huyo wa zamani wa klabu ya Palermo ameifungia PSG mabao 198 katika mechi 292, lakini msimu hu amefunga mabao 14 pekee.

Tammy Abraham ambaye ndiye mshambuliaji tegemeo wa Chelsea, kufikia sasa amefunga mabao 22 wakati Olivier Giroud, aliye na umri wa miaka 33, akiwa na mabao mawili pekee.

Giroud kuondoka

Kumekuwa na tetesi kwamba Giroud yuko njiani kuondoka Stamford Bridge mwezi huu wa Januari.

Huenda Cavani akakaribishwa haraka kuchukua nafasi hiyo hasa baada ya Lampard kushuhudia vijana wake wakipoteza nafasi nyingi Jumamosi, walipocheza na Newcastle United iliyowachapa 1-0, hiki kikiwa kichapo cha nane ligini msimu huu.

“Tulicheza vizuri kuliko Newcastle lakini hatukufunga mabao kwa sababu hatujaleta wachezaji wapya kuongezea kikosi nguvu,” alieleza Lampard.

“Tumepoteza mechi kadhaa, hata mbele ya mashabiki wetu ugani Stamford Bridge na itabidi tujirekebisha haraka wakati huu tunapopigana kukwama ndani ya mduara wa nne-bora ili kushiriki kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Safu ya mashambulizi ni miongoni mwa sehemu nitakazofanyia mabadiliko ya dharura.”

Baada ya msimu mmoja na klabu ya Fenerbahce ya Uturuki kwa mkopo, winga wa Chelsea, Victor Moses anatarajiwa kujiunga na Inter Milan pia kwa mkopo.

“Victor anarejea, lakini tayari amepanga kujiunga na timu nyingine licha ya uvumi unaoendelea kutanda miongoni mwa mashabiki wetu,” kocha Lampard alisema.