Michezo

Cazorla aomba kuwa kocha msaidizi Arsenal

June 1st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SANTI Cazorla ametaka usimamizi wa Arsenal kumkubalia kurejea uwanjani Emirates ili asaidiane kocha Mikel Arteta aliyekuwa mchezaji mwenza na ‘rafikiye mkubwa’ kambini mwa kikosi hicho ‘kuijenga’ upya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Cazorla ambaye ni mzawa wa Uhispania, alibanduka Arsenal mnamo 2018 baada ya mkataba wake kutamatika rasmi.

Hadi kuondoka kwake, hakuwa amechezea Arsenal mchuano wowote tangu Oktoba 2016 kutokana na jeraha baya la misuli ya kifundo cha mguu.

Kubanduka kwake kimya kimya hakukustahiki mchezaji wa haiba yake aliyefunga jumla ya mabao 29 na kuchangia mengine 45 katika michuano 180 ndani ya jezi za Arsenal.

Akiwa Arsenal, Cazorla alisaidia kikosi hicho kutwaa mataji mawili ya Kombe la FA akicheza pamoja na Arteta ambaye amesema atakuwa radhi zaidi kuunga naye kwa mara nyingine kwa majukumu tofauti pindi atakapostaafu rasmi kwenye ulingo wa soka mwishoni mwa muhula huu.

“Kwa kweli sijui chochote ambacho nitakumbukiwa kwako Arsenal. Pengine mashabiki wanajua, ila mimi mwenyewe sifahamu. Nahisi kwamba nina mengi zaidi ambayo ninaweza kukifanyia kikosi hicho ninachokithamini sana katika kiwango cha kocha msaidizi wa mkurugenzi wa soka,” akasema Cazorla.

Baada ya kuondoka Arsenal, Cazorla, 35, alijiunga na kikosi chake cha zamani cha Villarreal nchini Uhispania.

Licha ya umri wake mkubwa, bado anatamba mno ugani na amefunga mabao 12 na kuchangia mengine saba katika jumla ya michuano 29 iliyopita kambini mwa Villarreal.

Kuimarika kwa fomu yake kila uchao ni miongoni mwa sababu zilizomshuhudia akipangwa katika timu ya taifa ya Uhispania kwa baadhi ya michuano ya kufuzu kwa fainali za Euro 2020 alizotamani sana kuzinogesha kabla ya kuangika daluga.

Fainali hizo kwa sasa zimeahirishwa hadi 2021 kutokana na janga la corona.