CBC yalemea wazazi

CBC yalemea wazazi

Na WANDERI KAMAU

GHARAMA ya elimu nchini imekuwa mzigo mkubwa kwa wazazi, wengi wakielezea hofu yao kwamba, huenda wakashindwa kulipa baadhi ya ada wanazoitishwa.

Wazazi na wadau mbalimbali waliozungumza na ‘Taifa Leo’ walisema, gharama hizo zimechangiwa zaidi na mahitaji mengi ya Mfumo wa Elimu Tekelezi (CBC), hasa gharama ya vitabu.

Wazazi pia wanalalamikia mpangilio mpya wa ratiba za masomo, ambapo wanafunzi wamekuwa wakienda kwa likizo fupi fupi baada ya shule kufungwa kwa karibu miezi kumi mwaka uliopita kutokana na janga la corona.

“Tunapitia katika hali ngumu mno. Likizo fupi ambazo wanafunzi wanapewa hazituruhusu kupata muda wa kutafuta karo. Mwaka huu pekee, nimelipa karo mara tatu. Nitalipa mara ya nne Oktoba kwa kuwa wanafunzi watarejea shuleni kuanza muhula mpya,” akasema Bi Jackline Wambua, ambaye ni mkazi wa Nairobi.

Kulingana na ratiba ya Wizara ya Elimu, wanafunzi wataanza rasmi muhula wa kwanza wa 2021, Oktoba 9, baada ya kufunga shule Oktoba 1.

Wazazi wanasema haijakuwa rahisi kwao kulipa karo mara nne kwa mwaka mmoja, hasa wakati huu wanajaribu kurejelea maisha yao ya kawaida baada ya kuathiriwa vibaya na makali ya corona.

Kwa wanafunzi wanaojiunga na Gredi 4, wanahitajika kununua karibu vitabu kumi na vifaa vingine kama kalamu na madaftari ya kuchorea.

Hili linalenga kuwasaidia kufanya kazi za ziada ambazo wanapewa na walimu wao wanapoelekea shuleni.

Mzazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa alisema gharama ya vitabu hivyo ni ya juu mno kiasi kwamba, alilazimika kumhamishia mwanawe shule nyingine.

“Nilipoenda katika shule alikokuwa akisomea mwanangu nilipewa orodha ya vitabu vilivyonigharimu jumla ya Sh6,000. Nilishindwa namna ya kufanya kwa kuwa kiwango hicho hata kinazidi kodi ya nyumba ninayoishi,” akasema.

Katika hali hiyo, baadhi ya wadau wanasema kuwa huu ndio wakati mwafaka kwa serikali kutathmini tena mwelekeo iliochukua kuhusu utekelezaji wa mfumo huo, kwa kuwa mbali na kugeuka mzigo kwa wazazi wengi, taasisi muhimu kama vyuo vikuu bado havijajitayarisha kuutekeleza.

Kwenye mahojiano, wadau hao wanakosoa utekelezaji wake wakisema, uliharakishwa bila hata kuwapa wazazi nafasi ya kuutathmini ili kuuelewa kwa undani.

“Wazazi wengi wamejipata kwenye njiapanda kwani huu ni mpango ambao ulitekelezwa kwa kuharakishwa sana. Ingawa kulikuwa na vikao kadhaa vya kujadili utekelezaji wake, ni wadau wachache mno walishirikishwa. Kinaya ni kuwa, idadi kubwa ya wale walishirikishwa ni watu wasiotelekeza majukumu muhimu katika sekta ya elimu. Wengine hata wameanza kuukosoa,” asema Dkt Wandia Njoya, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya elimu.

Huku ikiibuka huenda wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu wakakosa kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) kwa muda ufaao, wadau wanasema huu ndio wakati wa kutathmini upya uongozi wa sekta hiyo muhimu.

“Malalamishi haya yote yanapaswa kuzindua serikali na kuilainisha sekta hii. Ni makosa wakati wazazi wanashindwa kugharimia ada za msingi ambazo watoto wao wanaitishwa shuleni. Elimu inapaswa kuwa haki ya msingi wala si chanzo cha malalamishi,” asema Dkt Njoya.

Hata hivyo, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, anasisitiza wizara hiyo imo katika mstari wa mbele kushughulikia matatizo yote yanayochipuka.

You can share this post!

Vihiga Queens kufufua uadui na CBE ya Ethiopia kwenye...

Franck Ribery ajiunga na Salernitana ya Italia akiwa na...