Habari Mseto

CBK kushirikiana na benki za kigeni kunasa wafisadi

June 20th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Patrick Njoroge Alhamisi amesema kuwa benki hiyo inashirikiana na benki kuu za mataifa ya Afrika Mashariki (EAC), Afrika na ulimwengu kwa jumla kuchunguza Wakenya wanaobadilisha sarafu za Kenya.

Hii ni katika jitihada za benki hiyo za kuwakamata wale ambao wanajaribu kulangua pesa walizoiba kutoka humu nchini kabla ya kutimia kwa Oktoba 1, 2019 siku ya mwisho ya kuondolewa kwa noti zote za zamani za Sh1,000.

“Tunawasiliana na benki kuu duniani, zikiwemo zile za mataifa ya Afrika Mashariki, kufuatilia ikiwa kuna Wakenya ambao wanawabadilisha pesa za Kenya kupitia benki hizo. Tumeziomba kuchukunguza kwa makini pesa zinazotoka taifa letu. Benki hizo zimekubali kushirikiana nasi,” Dkt Njoroge akaambia kikao cha wanahabari Alhamisi jijini Nairobi.

Gavana huyo alisema CBK imechunguza mchakato wa ubadilishanaji wa sarafu ulivyooendeshwa nchini India na kuweka mikakati ya kuzuia athari zinazotokena na zoezi hilo kama vile kupannda kwa mfumko wa bei za bidhaa.

Vile vile, Dkt Njoroge alitangaza kuwa makataa ya Oktoba 1, 2019 ya kuzimwa kwa matumizi ya noti za zamani za Sh1,000 hayatasongezwa.

“Tunataka kukamilisha shughuli hiyo tarehe mosi Oktoba ili kutoa nafasi kwa mashirika ya fedha na watu binafsi kuendesha shughuli zao kama kawaida. Kwa hivyo, hatutaongeza muda uliowekwa,” akasema.

Dkt Njoroge alisema kampeni za kuwahamasisha Wakenya kuhusu sarafu mpya zimekuwa zikiendeshwa kupitia vyombo vya habari na mabango ambayo yamewekwa katika vituo vyote vya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu, benki na taasisi za serikali.

“Na ili kuwafikia watu wengi, tumekuwa tukipeperusha jumbe zingine kuhusu sarafu mpya kupitia redio na televisheni. Na mnamo Jumatano tulianzisha apu inayotoa maelezo kuhusu yaliyomo kwenye sarafu mpya,” akaeleza.

Mnamo Juni mosi wakati wa sherehe za kitaifa za Madaraka Dei katika Dkt Njoroge alitangaza kwamba kuanzia Oktoba mosi note mpya za Sh1,000 ndizo zitakuwa zikitumika. Kwa hivyo, alitangaza kuwa wale wenye note za zamani waziliwasilishe kwa benki zilizo karibu kabla ya siku hiyo.

Alisema hatua hiyo ni njia mojawapo ya kupambana na tabia ya Wakenya kuficha nyumbani pesa walizopata kwa njia ufisadi badala ya kuzihifadhi katika benki kufuatia sheria kali zilizoanzishwa na CBK kufuatilia utoaji na uwekaji wa pesa katika benki.

“Kuanzia Oktoba 1, 2019 noti zote za Sh1,000 ambazo hazitakuwa zimerejeshwa zitakoma kutambuliwa kama pesa halali,” akasema Dkt Njoroge katika uwanja wa michezo wa Narok.